Chungana na marafiki wasikuvurugie ndoa
MARAFIKI ni sehemu muhimu katika ndoa. Wana uwezo wa kukujenga au kukubomoa kabisa.
Na sio kila rafiki ana nia njema. Wapo ambao wana ushauru wa kukusaidia kujenga ndoa yako, lakini pia wapo wanaotamani ndoa yako isambaratike.
Kuna ndoa nyingi zilikovunjika kwa sababu ya ushauri mbaya kutoka kwa marafiki. Baadhi ya wanandoa hujikuta wakifanya maamuzi ya kifamilia kulingana na maneno ya marafiki badala ya kuzungumza wao wenyewe.
Hii ni hatari kubwa kwa sababu urafiki si agano la ndoa, bali ndoa ni kati ya watu wawili tu – mume na mke.
Mshauri wa familia, Bw Daniel Muriuki, anasema wanandoa wanapaswa kuwa makini sana na aina ya marafiki wanaowaweka karibu.
“Rafiki wa kweli ataheshimu mipaka ya ndoa yako na hataleta fitina. Lakini rafiki asiye na nia njema atapanda mbegu za shaka na kusababisha nyie wawili kugombana,” asema Muriuki.
Kuna marafiki ambao hupenda kutoboa siri walizoambiwa, na wengine hutumia nafasi hiyo kuingilia ndoa za wengine. Kwa mfano, mume anaposota na rafiki yake si mwaminifu, habari hiyo inaweza kuenea na hata kufika kwa mke kwa njia ya umbea, na kusababisha hofu na mashaka yasiyo na msingi.
Bw Muriuki anawashauri wanandoa kuzungumza kwanza wao wenyewe kabla ya kutafuta ushauri nje. Ikiwa msaada wa nje unahitajika, ni vyema kumshirikisha mshauri wa kitaalamu.
“Rafiki wa kweli ni ndugu wa dhiki.” Hii ni ishara kwamba rafiki anayestahili ni yule anayelinda heshima ya ndoa yako, si yule anayekufurahia mkipigana.”
Kila ndoa inahitaji hekima ya kutambua ni nani wa kushirikishwa na mambo ya ndani. Hii si kusema wanandoa wajitenge kabisa na marafiki, bali wajifunze kuchuja.
“Rafiki anayewaunganisha na kuimarisha ndoa yenu anastahili kupewa nafasi. Lakini anayepanda shaka na uhasama anapaswa kuwekwa mbali,” anaongeza.
Anasema kuwa mwisho wa siku, ndoa ni safari ya wawili, na mtu wan je anabaki kuwa mgeni.
“Jihadharini na marafiki kwa sababu mara nyingi, fitina huanzia kwao.”