Makala

AI kukuza biashara ya kimataifa kwa asilimia 40 ifikapo 2040 -Ripoti

Na WINNIE ONYANDO September 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RIPOTI ya mpya ya Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) inaonyesha kuwa biashara kimataifa itatawaliwa na teknolojia ya AI (Artificial Intelligence) ifikapo 2040.

Ripoti hiyo inasema kuwa hii itawezekana tu iwapo mataifa yataziba pengo la kidijitali na kukumbatia teknolojia ya kisasa kama vile AI.

Ripoti ya mwaka huu ya World Trade Report 2025 inaonyesha kuwa biashara ya kimataifa inaweza kukua kwa kati ya asilimia 34 hadi 37 huku pato la taifa (GDP) likipanda kwa hadi asilimia 13 katika kipindi cha miaka 15 ijayo.

Ukuaji huo utachochewa na tija kubwa na gharama nafuu za biashara zitakazotokana na matumizi ya teknolojia ya AI.

Ripoti hiyo pia inasisitiza kuwa biashara inaweza kusaidia AI kukua kwa njia shirikishi kupitia upatikanaji wa bidhaa muhimu kama vile malighafi.

Mwaka 2023 pekee, bidhaa hizi zilikadiriwa kufikia thamani ya Sh294 trilioni.

Mkurugenzi Mkuu wa WTO, Bi Ngozi Okonjo-Iweala, alisema AI ina “uwezo mkubwa wa kupunguza gharama za biashara na kuongeza tija,” lakini akaonya kuwa ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa teknolojia unaweza kuongeza pengo la kiuchumi na kijamii.

“AI inaweza kufungua fursa mpya za ukuaji kwa mataifa yote,” alisema, akisisitiza kuwa kuziba pengo la kidijitali, kuwekeza katika ujuzi na kudumisha kanuni thabiti za biashara ni muhimu ili kuhakikisha ukuaji wa pamoja.

Ripoti imeonya pia kuwa vizuizi vya biashara vinavyohusiana na AI vimepanda kwa kasi – kutoka 130 mnamo mwaka 2012 hadi kufikia karibu 500 mwaka 2024, hasa katika mataifa yaliyoendelea na yale ya kipato cha kati.

Nchi za kipato cha chini bado zinakabiliwa na ushuru wa forodha wa hadi asilimia 45, hali inayozuia zaidi upatikanaji wa teknolojia muhimu.

Ili kuzuia ongezeko la tofauti kati ya nchi tajiri na maskini, WTO imetoa wito kwa serikali kuwekeza katika elimu, mafunzo ya ujuzi na sera za soko la ajira huku zikiboresha sheria za biashara ili kuendana na enzi ya kidijitali.