Wakazi wachoka na jiji wakilia kupanda kwa gharama ya huduma
Takribani mwaka mmoja baada ya Eldoret kupandishwa hadhi na kuwa jiji, wakazi wake sasa wanahisi mzigo wa kifedha baada ya Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Eldoret kuidhinisha ongezeko la asilimia 300 la bili za maji lililopendekezwa na kampuni ya maji ya jiji hilo, Eldowas.
Mahakama ilitupilia mbali ombi la kupinga nyongeza hiyo lililowasilishwa na wakazi wawili, Bw Kipkorir Menjo na Bw David Chebet kwa misingi kwamba lilikiuka Sheria ya Maji na kwamba mahakama haina mamlaka ya kushughulikia suala hilo. Hii inaipa Eldowas ruhusa ya kutekeleza viwango vipya vya malipo.
Kwa sababu hii, wakazi wa Eldoret sasa watalazimika kulipa mara tatu zaidi kwa maji kuliko walivyokuwa wakilipa kabla ya mji huo kuwa jiji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Eldowas, Dkt Lawrence Tanui, ongezeko hilo ni muhimu ili kufadhili mradi wa maendeleo ya miundombinu ya maji wa thamani ya Sh2.2 bilioni, uliopitishwa na Bodi ya Kudhibiti Huduma za Maji (WASREB).
“Tunatekeleza ongezeko hilo kwa kuzingatia mwongozo wa WASREB na taratibu za kuwajulisha wateja,” alisema Dkt Tanui.
Aidha, alisema wanatafuta ufafanuzi wa kisheria kabla ya utekelezaji rasmi, huku akiwahakikishia wateja huduma bora zaidi.
Licha ya hadhi mpya ya jiji, wakazi wanasema hali ya huduma za maji zimezidi kuwa mbaya huku yakikatika mara kwa mara na mifumo mibovu ya mitaro ya maji taka.