Makala

Umbea, adui wa ndoa imara

Na WINNIE ONYANDO September 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA jamii zetu, umbea umegeuka silaha inayobomoa ndoa nyingi.

Kuna wanaoamini umbea kutoka kwa majirani na marafiki kuliko wake au waume zao.

Lakini ukweli ni kwamba mara nyingi, porojo hizi hazina msingi wowote na zisipokomeshwa, zinaweza kuharibu uhusiano uliokuwa thabiti.

Wanandoa wengi wamejikuta wakigombana nyumbani kwa sababu ya umbea.

Kuna wanaodaiwa kusalitiwa, wengine kutuhumiwa kwa mambo ya kifamilia au kifedha, ilhali yote ni porojo zisizo na ukweli.

Tatizo ni kwamba baadhi ya wanandoa hufanya kosa la kuamini wanachosikia badala ya kuzungumza na wenzao moja kwa moja.

Mshauri wa masuala ya ndoa na familia, Bw Michael Nyawira anasema siri ya kulinda ndoa kutokana na umbea ni mawasiliano ya wazi.

“Wanandoa wakijifunza kuaminiana na kuzungumza bila kuficha, hakuna maneno ya mtu wa nje yatakayosababisha mgawanyiko. Umbea huota mizizi pale ambapo pana pengo la mawasiliano,” anasema Bw Michael.

Kando na hayo anawashauri wanandoa kujiepusha na watu wanaojulikana kwa kusambaza habari za uongo.

Anasema ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha ndoa yake inalindwa dhidi ya uvamizi wa maneno ya nje. Hii inamaanisha kuweka mipaka thabiti na marafiki au ndugu wanaopenda kuingilia masuala ya ndani ya familia.

“Marafiki au ndugu wa aina hii mara nyingi huleta sumu katika ndoa kwa kujifanya washauri ilhali nia yao ni kuona ndoa ikivunjika.

“Kumbuka, mchawi mkubwa ni jirani.”

Hii ni ishara kwamba wakati mwingine fitina kubwa huanzia karibu.

Aidha, ni vyema kukumbuka kwamba ndoa ni kati ya watu wawili tu – mume na mke. Wengine wote ni watazamaji. Mnapokabiliana na changamoto, Bwa Michael anasema wanandoa wanafaa kusuluhisha tofauti zao nyumbani badala ya kupeleka matatizo yao kwa kila mtu.

“Kila mnapopeleka siri za ndoa nje, mnaipa nafasi kwa umbea kuimarika.”

Mshauri huyo anasema kuwa kila ndoa ina changamoto zake, na hakuna uhusiano usio na majaribu. Lakini hekima ni kusimama pamoja kama wanandoa na kushinda changamoto hizo kwa upendo na heshima.

“Umbea hautakosa, ila nguvu zenu zikiwa kwenye kuaminiana na kuelewana, ndoa yenu haitatikiswa,” anaongeza.

Usikubali tetesi zisizo na ukweli zikuvunjie ndoa. Mpe mwenzako nafasi ya kujieleza na msikilizane. Mwisho wa siku, nyie wawili ndio mnajua ukweli wa nyumba yenu.