Sonko afunguka, atangaza atagombea ugavana 2027
ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Gideon Mbuvi Sonko, mnamo Ijumaa alifichua kwa hisia kali jinsi alivyolengwa na serikali kumuangamiza kisiasa, huku akitangaza nia yake ya kuwania tena ugavana mwaka wa 2027.
Bw Sonko alikanusha madai kuwa safari yake ya kisiasa imefika kikomo, akisisitiza kuwa bado hajamaliza kazi yake ya kisiasa.
Alidokeza kuwa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki hivi karibuni itamuondolea lawama kwa kutoa uamuzi anaosema ulikataliwa na mahakama za humu nchini.
Aliyasema hayo wakati wa sherehe ya mahafali ya rafiki yake wa karibu, Elkana Jacobs, anayewania ubunge wa Nyali, hafla iliyofanyika Nairobi.
Katika hotuba ya kipekee, Bw Sonko alidai masaibu yake ya kisiasa hayakusababishwa na makosa yake, bali na hasira ya serikali kuu dhidi ya msimamo wake mkali wa kupinga ufisadi.
Sonko alikumbuka kuwa alipokuwa gavana, Sh60 milioni ziliwasilishwa kwa ofisi yake kama hongo. Badala ya kuzipokea, alisema aliarifu mamlaka husika.
Maafisa wa ujasusi walipelekwa ofisini mwake, kamera zikawekwa, na muda mfupi baadaye pesa hizo zikawa zinaletwa kila wiki.
“Tuliweka kamera kila mahali, na kila wiki mtu yule yule alikuwa analeta kiasi kilekile cha pesa,” alieleza Sonko.
“Hapo ndipo serikali ilikubali kuanzisha mfumo usiotumia pesa taslimu ili kudhibiti wizi wa pesa za umma, nami nikauunga mkono. Baadaye, mapato yote yalipelekwa moja kwa moja kwa Benki Kuu ya Kenya.”
Hata hivyo, alidai kuwa hatua hiyo ilikuwa mwanzo wa masaibu yake. Badala ya kupongezwa kwa uwazi, alisema serikali iligeuka dhidi yake na kumshutumu kwa ubadhirifu wa pesa hizo.
“Nilikuwa mjinga wakati huo. Nilifuata tu bila kujua. Alikuwa rafiki yangu wa karibu na sikuwahi kufikiria angenigeuka na kufanya alivyofanya,” alisema bila kutaja jina la mtu.Alikumbuka pia kuwa maafisa wenye nguvu serikalini walimwambia “apunguze kasi.”
Miradi kama ukarabati wa mitaa ya Woodley na Ziwani, na ujenzi wa masoko katika Dagoretti North na Kang’undo, alisema haikukaribishwa bali ilionekana kama changamoto kwa serikali kuu.
“Nilipigiwa simu na katibu mwenye ushawishi mkubwa na akaniambia nafanya kazi haraka kuliko serikali kuu, jambo lililowafanya waonekane wabaya,” alisema Sonko.
“Walitaka nipunguze kasi.”
Alipokataa, mchakato wa kumbandua kupitia bunge la kaunti ulianza.Aliongeza kuwa baada ya kuondolewa mamlakani, alipewa Sh70 milioni na kuambiwa ahamie Mombasa ambapo Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka angemsaidia kuwania ugavana wa kaunti hiyo.
Hata hivyo, alidai kuwa watu serikalini waliomwondoa Nairobi waligeuka dhidi yake Mombasa baada ya kuona anaelekea kushinda.
“Nilishangaa Mahakama ya Juu iliponipiga marufuku kuwania, na nikaondolewa kwenye orodha ya wagombea ugavana wa Mombasa.
Ilikuwa ni uchungu mwingi lakini sikukata tamaa,” alisema.Sonko alielekea Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), akidai kuwa mahakama za Kenya—hasa Mahakama ya Juu—zilikiuka Katiba pamoja na misingi ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.