Kimataifa

Kura yapigwa kuruhusu mkuu wa jeshi kuwania urais baada ya mapinduzi ya serikali

September 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CONAKRY, GUINEA

MATOKEO ya kura ya maamuzi iliyoanza jana yanaweza kumruhusu kiongozi wa jeshi lililofanya mapinduzi nchini kuwania urais na inaangaziwa kwa kina eneo hilo lililoathirika zaidi na mapinduzi.

Raia wa taifa hili la pwani wanapiga kura kuunga mkono au kupinga rasimu mpya ya katiba, ambayo ni hatua muhimu ya kuhamisha taifa kutoka utawala wa kijeshi na kuingia utawala wa raia. Uchaguzi unatarajiwa kufuata Desemba.

Guinea ni moja kati ya nchi za Afrika Magharibi, zikiwemo Mali, Niger na Burkina Faso, ambazo majeshi yametwaa mamlaka na kuchelewesha utawala wa raia.

Wakosoaji wanasema kura ya maamuzi iliyofanyika jana ni njia ya Jenerali Mamadi Doumbouya, aliyemng’atua mamlakani Rais Alpha Conde kusaka urais na kuhalalisha utawala wake wa kijeshi.

Jenerali Doumbouya aliangusha serikali 2021 na kuapa kurejesha taifa kwa utawala wa raia kufikia mwisho wa mwaka uliopita.

Kuna wapigakura 6.7 milioni walioidhinishwa na kura ya maoni inahitaji angalau asilimia 50 kujitokeza ili ipitishwe.

Katika siku za mwisho wa kampeni, jiji kuu la Conakry lilifurika shughuli tele ikiwemo masomo ya kuran, tamasha za muziki wa reggae na maombi yaliyofanyika kwa wanaopigia debe ‘ndio’ kumuunga mkono Doumbouya.

Wafuasi waliovalia tishati na mavazi ya kitamaduni ya Afrika Magharibi yaliyochorwa sura ya Doumbouya walikusanyika kwenye mikutano ya hadhara lakini upinzani haukuwepo.

Kampeni zilipigwa marufuku Ijumaa na Jumamosi lakini kura ya maoni ikaendelea.

Majengo ya umma na ya kibinafsi jijini Conakry yalisalia kubandikwa mabango ya “ndio” yakipigia debe kupitisha kura ya maoni.

Utawala wa kijeshi ulinyamazisha wakosoaji mwaka uliopita na kuvunjilia mbali vyama vya kisiasa zaidi ya 50 katika hatua iliyodai ilikuwa “kusafisha uwanja wa kisiasa.”

Wiki chache kabla ya kura ya maoni kifanyika, utawala wa kijeshi ulisimamisha vyama vitatu vikuu vya upinzani na kuvizuia kuandaa mikutano ya hadhara na kuzungumzia wananchi.

Zaidi ya nusu ya raia nchini humu hawawezi kusoma wala kuandika, kumaanisha namna pekee wanayopata habari kuhusu katiba mpya ni kutoka kambi ya “ndio,” alisema Rafiou Sow, rais wa chama cha upinzani cha Renewal and Progress Party, moja kati ya vyama vya kisiasa vilivyosimamishwa, aliyehimiza kususia kura hiyo ya maoni.

“Wanaharakati na wafuasi wetu hawana uelewa wa katiba hii. Mara tu tulipotengwa, walitengwa,” alisema.

“Sisi, tuliopaswa kusaidia rai awa Guinea kuelewa kilichoandikwa ndani yake, tulipigwa marufuku hata kuzungumza.”

Doumbouya alitwaa mamlaka kimabavu miaka minne iliyopita, akisema alifanya hivyo kuzuia taifa kutumbukia kwenye machafuko akikashifu serikali iliyopita kwa ahadi zilizovunjwa.

Licha ya utajiri wa maliasili, zaidi ya nusu ya raia 15 milioni nchini wanakabiliwa na “viwango vya juu kupindukia vya ufukara na ukosefu wa chakula,” kulingana na Mpango wa Chakula Duniani.

Awali, Doumbouya alisema hatawania urais. Lakini rasimu ya katiba inaruhusu wanajeshi kugombea afisi na kurefusha mihula ya urais kutoka miaka mitano hadi saba, inayoweza kuwania mara mbili.

Japo Doumbouya hajasema hadharani kuhusu iwapo atagombea uchaguzi Disemba, amesalia kigogo katika kampeni ya kura ya maoni.