Kimataifa

Tshisekedi amruka Trump, asema DR Congo haitaipa Amerika madini yake

Na REUTERS September 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NEW YORK, AMERIKA

RAIS Felix Tshisekedi, Jumatatu alisema nchi hiyo haitanadi madini yake kwa Amerika kutokana na juhudi ambazo zimekuwa zikiendelezwa kusaka amani mashariki mwa DR Congo.

Tshisekedi amemshukuru Rais Donald Trump kwa juhudi hizo japo akasema Amerika haijafaulu kumaliza uhasama kati ya M23 na wanajeshi wa DR Congo.

Mnamo Juni 27, Amerika ilifaulu kupatanisha DR Congo na Rwanda kama sehemu ya kumaliza uhasama huo. Kuna madai kuwa Kundi la M23 limekuwa likifadhiliwa na serikali ya Rwanda.

Makataa ya kutekeleza muafaka huo ni mwisho wa mwezi huu.Amerika imekuwa ikiendeleza juhudi za kupatanisha nchi hizo ili inufaikie madini mbalimbali ambayo yapo mashariki mwa DR Congo.

“Hatujanadi wala hatutanadi madini yetu bali tunamakinikia kuimarisha sekta ya madini na kuimarisha miundomsingi pamoja na kawi,” akasema Tshisekedi akizungumza na wanahabari jijini New York.

Kama mbinu inayoweza kufasiriwa kama kuruka Amerika, Tshisekedi alifichua kuwa nchi hiyo imetia saini mkataba na China wa kuimarisha sekta yake ya kawi.

Hata hivyo, hakufichua mengi kuhusu yaliyomo kwenye mkataba huo.

Maafisa wa DR Congo wamekuwa wakisema kuwa kufaulu kwa muafaka wa amani uliotiwa saini unategemea iwapo Rwanda itakoma kufadhili M23.

“Rwanda ilituhadaa inawaondoa wanajeshi wake lakini bado inawaongeza na inawaendelea kuwapiga jeki,” akasema Tshisekedi.

Mnamo Machi, Qatar ilifaulu kuandaa kikao kilichomshirikisha Rais Paul Kagame wa Rwanda na Tshisekedi ambapo viongozi hao wawili walitoa wito wa kusitishwa kwa vita.

M23 imesema kuwa inawataka wafungwa waachiliwe huru kabla ya mazungumzo kuanza.

DR Congo nayo inasisitiza kuwa itawaachilia tu wafungwa baada ya muafaka kutiwa saini. Agosti 18 ndiyo ilikuwa makataa ya kutia saini makubaliano hayo.