Habari za Kitaifa

Wabunge warai Amerika irefushe mkataba wa Agoa

September 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Bunge la Kitaifa limetoa wito wa kuharakishwa kwa mazungumzo ya kurefusha Mkataba wa Ukuaji wa Kiuchumi na Fursa kwa Afrika (AGOA).

Katika hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Laikipia, Bi Jane Kagiri na kuungwa mkono na wabunge kutoka mirengo yote ya kisiasa, wabunge walisisitiza umuhimu wa AGOA na jinsi inavyonufaisha taifa kwa kiasi kikubwa.

Bi Kagiri alielezea wasiwasi wake kuhusu muda wa sasa wa mkataba huo wa AGOA, uliorefushwa mwaka wa 2015 na unatarajiwa kuisha mwezi Septemba mwaka huu, akionya kuwa kutorefusha muda huo kutaathiri uchumi wa Kenya kwa kiwango kikubwa.

“Wanawake wanawakilisha takriban asilimia 75 ya walionufaika moja kwa moja na AGOA, na mapato yao husaidia kugharamia elimu, huduma za afya, na kupunguza umasikini,” alisema Bi Kagiri.

“Bunge hili linaitaka Serikali ya Kenya, kwa kushirikiana na Serikali ya Amerika kufuatilia kuongezwa kwa Mkataba wa AGOA kwa kipindi cha ziada cha miaka kumi na sita,” aliongeza Bi Kagiri.

Aliweka wazi kuwa upanuzi huo ni muhimu kulinda mafanikio ya kiuchumi, ajira, na kuimarisha uthabiti wa muda mrefu na ustawi wa bara la Afrika. Aidha, iwapo mkataba huo hautarefushwa, alisisitiza kuwepo kwa kipindi cha mpito cha miaka miwili ili kuandaa makubaliano mapya ya kibiashara ambayo yatahifadhi biashara na nafasi za ajira nchini Kenya na Amerika.

Wabunge walitaka Rais William Ruto ambaye kwa sasa yuko ziarani nchini Amerika, kuanzisha mazungumzo ya pembezoni kuhusu kurefusha AGOA.

Mwenyekiti wa Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria, Bw. George Murugara (Tharaka), alieleza kuwa mapato yanayotokana na AGOA ni muhimu kwa ujenzi wa uchumi na kuinua hali ya maisha ya Wakenya masikini.

“Kukomeshwa kwa AGOA hakutaathiri Kenya pekee, bali Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa ujumla. Ni lazima kuwe na makubaliano ya pande mbili ili kuimarisha uhusiano baina ya mataifa haya mawili. Tunafahamu kuna tofauti kubwa ya kiuchumi kati ya mataifa haya mawili,” alisema Bw. Murugara.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa makubaliano hayo kuhimiza uzalishaji wa bidhaa na viwanda ili kuepuka pengo la kiuchumi.

“Bw Spika, tungependa AGOA iendelee. Bila hilo, mataifa mengi yataathirika. Tunaomba Kenya na Amerika ziendelee kuwa na moyo wa huruma na kufikiria upanuzi wa AGOA,” alisema Bi Catherine Omanyo.

Bw. Owen Baya (Kilifi Kaskazini) alisifia mkataba wa AGOA kama sheria iliyoleta maendeleo makubwa na kuhimiza Afrika kuzalisha bidhaa kwa soko la Amerika.

“Kenya imenufaika pakubwa na AGOA, hasa kupitia viwanda vya EPZ na programu nyingine za ajira,” alisema Bw Baya.

Kwa mujibu wa hoja hiyo, AGOA imekuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara, kuvutia wawekezaji, na kuunda ajira, hasa kwa wafanyakazi wa kipato cha chini – hivyo kuimarisha uchumi na uthabiti wa kijamii.

“Tunaomba Rais wa Amerika Donald Trump, aunge mkono kuendelea kwa AGOA ili Kenya isipate hasara,” alisema Bw John Waluke (Sirisia).

Kwa mujibu wa hoja hiyo, kurefushwa kwa AGOA kutaendelea kukuza biashara na uwekezaji kati ya Amerika na mataifa ya Afrika yaliyohitimu.

Aidha, hoja hiyo ilibainisha kuwa AGOA ni ushindi kwa mataifa yote mawili, kwani pia imeinufaisha Amerika kwa kusaidia mfumo wa usambazaji, kuimarisha uhusiano wa kibiashara, na kuunganisha wafanyabiashara wa Amerika na fursa zilizopo chini ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).