Habari Mseto

Wakenya waumia huku serikali ikisema hali ni shwari, utafiti wasema

Na CHARLES WASONGA September 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAKENYA wengi wanahisi kwamba, taifa linaelekea mkondo mbaya huku wakisema changamoto kubwa ni gharama ya juu ya maisha na ukosefu wa ajira, matokeo ya utafiti yaliyotolewa jana yameonyesha.

Kulingana na utafiti huo ulioendeshwa na kampuni ya Infotrak, asilimia 57 ya wananchi waliohojiwa wanaamini Kenya inaelekea pabaya.

Kwa upande mwingine ni asilimia 17 pekee ya Wakenya wanahisi nchi inaelekea mkondo mzuri.

Jumla ya Wakenya 2400 walihojiwa katika utafiti huo ambao uliendeshwa kati ya Agosti 13 na Agosti 14, mwaka huu katika kaunti zote 47 na maeneo manane nchini.

Wale waliohojiwa, kwa njia ya simu, ni wenye umri wa miaka 18 kwenda juu, kulingana na kampuni hiyo ya Infotrak.

Kati ya Wakenya wanaohisi kuwa nchi inaelekea katika mkondo mbaya, asilimia 66 walitaja gharama ya juu ya maisha kama changamoto kubwa huku asilimia 30 wakihisi ukosefu wa ajira ndio kero kuu.

Changamoto zingine zinazowafanya raia kuhisi kuwa taifa linaelekea mkondo mbaya ni kama vile utawala mbaya (asilimia 15, kutofanyakazi kwa bima ya SHIF/SHA (asilimia 15), kukithiri kwa ufisadi (asilimia 14), changomoto katika sekta ya elimu (asilimia 11) huku asilimia nane kati yao wakitaja umasikini.

Masuala mengine yanayowafanya Wakenya kuhisi kuwa taifa linaelekea pabaya ni; ongezeko la mauaji ya kiholela, ubovu wa miundomsingi, ukabila, kukwama kwa miradi ya serikali, ongezeko la visa vya utovu wa usalama, utekaji nyara, miongoni mwa mengine.

Matokeo ya utafiti huo yametolewa wakati Rais William Ruto na wandani wake wamekuwa wakisifia utendakazi wa serikali wakitaja mikakati yake ambayo imechangia kupunguza kwa kiwango cha mfumko wa bei na kuimarika kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo.