WanTam nyingine yanukia Ushelisheli, Rais akishindwa na mpinzani awamu ya kwanza
VICTORIA, Ushelisheli
WAPIGA kura nchini Ushelisheli watarejea debeni kushiriki marudio ya uchaguzi wa urais baada ya washindani wawili wakuu kutopata angalau asilimia 50 ya kura, mamlaka ya uchaguzi imesema.
Kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa Jumapili, kiongozi wa upinzani Patrick Herminie aliongoza kwa kupata asilimia 48.8 za kura zilizopigwa na kuhesabiwa huku rais wa sasa Wavel Ramlalawan akimfuata kwa karibu kwa kupata asilimia 46.4.
Kulingana na sheria ya nchi hiyo, mgombeaji wa urais sharti apate asilimia 50 na kura moja, ndiposa atangazwe mshindi.
Hata hivyo, mamlaka ya kusimamia uchaguzi haikutangaza ni lini marudio ya uchaguzi yatafanywa
Japo shughuli ya upigaji kura ilianza Alhamisi wiki jana, Septemba 25, wapiga kura wengi walijitokeza Jumamosi.
Chama cha upinzani, United Sychelles Party (USP) kinachoongozwa na Herminie kiliongoza taifa hilo kabla ya kuondolewa mamlaka miaka mitano iliyopita.
Kiliongoza Ushelisheli kuanzia 1977 hadi 2020.
Katika jaribio la kuzuia USP kurejea mamlakani Rais Ramkalawan anatetea kiti chake akisaka nafasi ya kuendelea kuongoza kwa muhula wa pili kupitia chama chake, Linyon Domokratik Seselwa.
Amekuwa akiendesha kampeni zake kwa ahadi ya kufufua uchumi, kuchochea maendeleo ya kijamii na utunzaji wa mazingira.
Hata hivyo, chama cha Rais Ramkalawan kimekumbwa na upinzani mkali kuelekea uchaguzi mkuu ulioanza Alhamisi wiki jana.
Aidha, wanaharakati waliwasilisha kesi dhidi ya serikali wiki moja kabla ya uchaguzi kupinga uamuzi wa juzi wa kukodishwa kwa sehemu ya Kisiwa cha Assomption.
Serikali ilikodisha kisiwa hicho kikubwa zaidi nchini humo kwa kampuni moja ya Qata inayopania kujenga mkahawa wa kifahari hapo.
Kulingana na makubaliano kuhusu mpango huo, kampuni hiyo ingeupanua uwanja wa ndege katika kisiwa hicho ili uhudumie ndege kutoka mataifa ya kigeni.
Makubaliano hayo yalikumbwa na upinzani mkali, wanaharakati wakisema unafaidi wageni wala sio raia wa Ushelisheli.
Wapiga kura wengi pia walichukizwa na kukithiri kwa matumizi ya mihadarati aina ya heroine. Inakadiriwa kuwa jumla ya watu 6,000 kati ya idadi jumla ya watu 12,000 nchini Ushelisheli wanatumia dawa hiyo ya kulevya.
Rais Ramkalawan analemewa na mpinzani wake siku chache baada ya Rais wa Malawi Lazarus Chakwera kubwagwa na mpinzani wake mkuu Peter Mutharika.