Mpango wa Huduma Namba wazinduliwa Thika
Na LAWRENCE ONGARO
MPANGO wa kusajili wananchi wa Huduma Namba ambao unaendeshwa kwa njia ya kidijitali, ulizinduliwa rasmi Jumatatu mjini Thika, na makatibu wawili.
Katibu wa Kawi Mhandisi Patrick Njoroge, na wa fedha Dkt Kamau Thugge, waliandamana na Mbunge wa Thika, Mhandisi Patrick ‘ Jungle’ Wainaina walipozindua mpango huo katika eneo la Kiganjo, mjini Thika.
Dkt Thugge alieleza umuhimu wa mpango huo wa kujisajili akisema utaendelea katika kaunti zingine 15.
Baadhi ya kaunti zilizozindua mpango huko ni kama Nairobi, Kiambu, Uasin Gishu, Kapsabet, Kilifi, na Tana River.
“Mpango wa Huduma Namba, ni muhimu kwani utawasilisha maelezo yote ya mtu binafsi. Itasajili maelezo ya kitambulisho, pasipoti, leseni ya kuendesha gari, na mambo mengine muhimu,” alisema Dkt Thugge.
Aliwahimiza wananchi waukumbatie mpango huo kwani utazuia mambo mengi ya ulaghai ambao umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu.
Katibu wa Kawi Mhandisi Patrick Njoroge alisema kuwa serikali itafanya juhudi kukamilisha ajenda zake nne kwa muda wa miaka minne ijayo.
Alimshauri Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina kushirikiana na gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu na kujadiliana jinsi viwanda vichache vinaweza kufufuliwa ili vibuni ajira kwa vijana katika kaunti hiyo.
Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba wakazi wa Thika wanapata umeme hasa maeneo ya mashinani.
Aliwataka viongozi wa Kiambu wajadiliane na katibu wa afya ili kujenga hospitali ya kiwango cha Level 4 eneo la Kiganjo, Thika.
Bw Wainaina aliitaka serikali kuu ichukue jukumu la huduma za afya kutoka kwa Kaunti.
“Ningetaka hospitali kubwa ijengwe katika eneo hili la Kiganjo kwa sababu ina idadi ya wakazi wapatao 120,000.
Alipongeza mpango wa Huduma Namba ambao alisema utasaidia kutambua Wakenya halisi.
Alisema yuko tayari kuwasaidia wahudumu wa bodaboda ambao tayari wamejiweka katika makundi 37 mjini Thika.
Wakati wa uzinduzi wa Huduma Namba, machifu walihimizwa kuwa mstari wa mbele kuwahimiza wananchi kujisajili.
Makatibu hao wawili; Njoroge, Thugge na Mbunge wa Thika Bw Wainaina walikuwa watu wa kwanza kusajiliwa rasmi nao wakuu wengine wa serikali wakifuata mwito huo.