IEBC imeandikisha wapiga kura wapya 7,048 tu kwa siku sita
WAKENYA 7,048 pekee ndio wamejisajili kuwa wapiga kura wapya tangu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilipoanza rasmi zoezi la usajili mpya wa wapiga kura Jumatatu, wiki hii.
Kulingana na IEBC, idadi hiyo ni sawa na asilimia 0.11 ya lengo la kusajili wapiga kura wapya milioni 6.3 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa usajili wa wapiga kura wapya (1,597), ikifuatiwa na Mombasa (556), Kiambu (386), Kisii (312) na Machakos (260).
Kwa upande mwingine, kaunti zilizoshuhudia usajili mdogo zaidi ni pamoja na Lamu (1), Nyamira (10), Samburu (18), Tana River (21) na Tharaka Nithi (24).Naibu Rais, Prof Kithure Kindiki, ambaye anatoka Tharaka Nithi anarai wananchi kujitokeza kwa wingi kujisajili.
“Nawasihi wananchi kote nchini, kama huna kitambulisho pata kwanza, halafu upate kadi ya kura. Uwe tayari kufanya maamuzi kuhusu uongozi mnamo 2027,” alisema akiwa Ganze, Kaunti ya KilifiKatika Kaunti ya Busia (Teso Kaskazini) na Homa Bay (Karachuonyo), viongozi wa serikali wakiongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula pia walihimiza wakazi kujisajili.
IEBC inatarajia idadi ya waliojisajili itaongezeka kadri muda unavyoendelea, kwa kuwa Wakenya wengi kwa kawaida hujitokeza dakika za mwisho. Tume hiyo inasisitiza dhamira yake ya kuhakikisha kuwa usajili wa wapiga kura unaendelea kuwa wazi, shirikishi, wa kuaminika na bora kwa Wakenya wote.
Mwenyekiti wa IEBC Erastus Edung Ethekon aliwahimiza Wakenya wote, hasa vijana na wapiga kura wa mara ya kwanza, kujisajili ili waweze kushiriki uchaguzi mkuu wa 2027.“Tume inatoa wito kwa raia wote kutumia fursa hii kujisajili kama wapiga kura,” alisema Ethekon.