Siku za mwisho za Jomo Kenyatta kizuizini
KIFUNGO cha Jomo Kenyatta Lokitaung kilikamilika Aprili 14, 1959, lakini agizo la kumweka kizuizini lililotolewa na Jaji Thacker na kuidhinishwa na Gavana Baring mnamo Septemba 1954 liliendelea kutumika mara moja.
Kenyatta alihamishiwa Lodwar, mji mkuu wa wilaya ya Turkana Kaskazini, umbali wa takriban kilomita 144 kutoka Lokitaung. Majumba kadhaa yalikuwa yamejengwa tayari kuwazuilia Kenyatta na wenzake almaarufu The Kapenguria Six pindi kifungo chao kingekamilika.
Kenyatta alitaja hali ya Lodwar kuwa “aina tofauti ya kifungo.” Alipokea posho ya paundi sita kila mwezi, na aliruhusiwa kufanya ununuzi kwa saa mbili katika maduka mawili ya Wahindi aliyoekelezwa.
Hata hivyo, hakuruhusiwa kuzungumzia siasa na mtu yeyote wakati wa matembezi haya. Alieleza maisha ya Lodwar kuwa “ya kuchosha kabisa, ambapo joto na vumbi zilipiga kelele za haleluya kila siku.”Mwezi mmoja baada ya kuwasili, alijiunga na mkewe wa tatu, Mama Ngina, na binti zake wawili, ambao alikuwa hajawaona tangu Oktoba 1952.
Sikukuu ya Krismasi mwaka huo ilikuwa ya kipekee, kwani alitembelewa na ndugu yake James Muigai na binti yake Margaret Wambui.Kenyatta alikaa Lodwar kwa miaka miwili, akivumilia hali ya joto kali na mazingira magumu.
Mwaka wa 1960 ulileta matumaini mapya. Waziri Mkuu wa Uingereza Harold Macmillan, katika hotuba yake maarufu ya “Wind of Change” nchini Afrika Kusini mnamo Februari 3, alieleza kuwa:“Upepo wa mabadiliko unavuma barani Afrika, na iwe tunapenda au la, hali hii ya mwamko wa kisiasa ni ukweli wa kisiasa ambao sera zetu lazima zizingatie.”
Kifo cha wafungwa 11 wa MauMau katika kambi ya Hola Machi 3 1959 kilileta aibu kubwa kwa Uingereza, na kulingana na Waziri wa Masuala ya Koloni Iain Macleod, tukio hilo lilionyesha wazi kuwa mabadiliko ya haraka yalihitajika Kenya.
Katika Mkutano wa Lancaster House uliofanyika Januari 1960, Macmillan alidokeza kuwa nia yake ilikuwa ni kutoa utawala wa wengi kwa Waafrika nchini Kenya haraka iwezekanavyo.Aprili 14, 1961, Kenyatta alihamishwa kutoka Lodwar hadi Maralal, wilayani Samburu.
Hii iliashiria hatua ya mwisho ya kizuizi chake. Hapa ndipo serikali iliamua kuwa ni wakati wa Kenyatta kukutana tena na vyombo vya habari vya kimataifa, baada ya miaka minane tangu kesi ya Kapenguria.
Kwa wengi waliokuwa wakoloni, Kenyatta alihusishwa na harakati za MauMau, na walimchukulia kama mtu hatari. Lakini alipoonekana kwenye kamera akiwa amevalia koti la ngozi, na akizungumza Kiingereza kwa sauti tulivu na kwa utulivu, alieleza kuwa amekuwa akitengwa kwa miaka minane na hivyo alikuwa ametengwa na dunia na siasa za wakati huo.
Aliwasihi wanahabari wawe wa kweli katika taarifa zao na waepuke uzushi au habari za kupotosha.Kipindi cha miezi minne Maralal kilimwezesha Kenyatta kukutana na viongozi mbalimbali wa kisiasa, dini, jamii tofauti, marafiki, madaktari, wanasheria, wapigapicha na hata viongozi wa kimataifa.
Wote waliomtembelea waliondoka na msimamo mmoja kwamba“Kenyatta ndiye kiongozi wa kuhakikisha haki za wote zitalindwa katika Kenya huru.”Miongoni mwa waliomtembelea alikuwa Michael Blundell, ambaye Kenyatta alimhakikishia kuwa hana chuki yoyote dhidi ya Wazungu na kwamba wakulima wa kizungu ni muhimu kwa uchumi wa Kenya.
Mnamo Agosti 14, 1961, Kenyatta aliruhusiwa kurudi nyumbani Gatundu. Baada ya wiki moja ya kizuizini nyumbani, alikutana na Gavana katika afisi ya Mkuu wa Wilaya (DC), ambapo alikabidhiwa pete yake na fimbo yake nyeusi ya mbao, ishara ya mwisho ya kuwa huru kabisa.Baada ya hapo, Kenyatta alifanya mikutano ya ushindi kote nchini.
Mnamo Oktoba 28, 1961, alikubali kuwa Rais wa Kanu, na Novemba 26 alifanyiwa mahojiano na BBC kwenye kipindi cha Face to Face.Kenyatta hakutazama nyuma tena – aliongoza taifa kuelekea uhuru rasmi mwaka 1963, na kuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Kenya mwaka 1964.