• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Gatundu Kusini: Wahalifu wanaolenga vichwa vya watu kwa vifaa butu na kuwaua

Gatundu Kusini: Wahalifu wanaolenga vichwa vya watu kwa vifaa butu na kuwaua

NA MWANGI MUIRURI
HALI ya wasiwasi imezidi kutanda katika Kaunti Ndogo ya Gatundu Kusini, kufuatia kukithiri kwa visa vya wahuni kuvamia rai ana kuwaua.

Katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, takwimu za idara ya ujasusi nchini zinaonyesha kwamba watu 12 wamepoteza maisha yao kupitia uhalifu.

Idadi hiyo ni pamoja na watu wanne ambao hivi majuzi walivamiwa wakielekea nyumbani, na kila mmoja kugongwa kichwani kwa kifaa butu hadi kufa

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kiambu, Bw Perminus Kioi, wanne hao walikuwa wakielekea nyumbani mnamo Agosti 21, 2023 walipokumbana na mauti.

“Ni katika kijiji cha Gacugi mwendo wa saa tatu usiku kuliposikika vurumai barabarani kabla ya majirani kuamkia mauti hayo. Tayari tumekamata mshukiwa mkuu na ameshtakiwa,” akasema.

Eneo hilo maarufu kwa biashara ya pombe za mauti na mihadarati, limekuwa na changamoto za kuzorota kwa usalama hasa katika vijiji vya Kairi, Ngorongo, Kagambwa na Gatono.

Wenyeji wamekuwa wakilalamikia visa vya uvamizi katika biashara na makazi huku vitengo vya kiusalama vikidaiwa kuzama katika hongo za washukiwa wa uhalifu.

Wenyeji walisema wanahangaika mikononi mwa wahalifu ambao kando na kuwaua, huwa wanawaibia mifugo, mimea na mavuno.

“Ni kumaanisha wakora hapa hawaheshimu kamwe vitengo vya kiusalama. Ikiwa wakora wanaweza kupita barabara kuu wakiwa wamejihami na kisha waue watu wanne ina maana kwamba hakuna hofu kwa maafisa wa usalama wanaojielewa,” akasema Bw Stephen Ndaki, mtaalamu wa masuala ya kiusalama.

Bw Kioi alisema kwamba kisa hicho kinachunguzwa kwa umakinifu na hivi karibuni mambo yatajidhihirisha.

Mbunge wa eneo hilo, Bw Elijah Kinyanjui tayari ametoa ilani kwa maafisa wa usalama waimarishe hali ya usalama.

Alisema eneo hilo limetelekezwa kwa kuhusishwa na eneobunge la Gatundu Kusini ambako Rais wa kwanza na wa nne nchini wakiwa ni; baba na mwanawe (Mzee Jomo Kenyatta na Uhuru Kenyatta) mtawalia walitoka.

“Huku maendeleo mengi yalienda upande wa Kusini, eneo hili letu lilibakia nyuma na ndiyo sababu hata usalama umezorota,” akasema.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Didmus Barasa: Tulipopeleka Raila Bondo, tulipaswa kuweka...

Gavana akanusha watoto 5 walifariki umeme ulipopotea

T L