Kimataifa

Magaidi washambulia jela lenye ulinzi mkali jiji kuu la Mogadishu

Na REUTERS October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MOGADISHU, SOMALIA

VIKOSI vya usalama vilipigana vikali Jumamosi kufurusha wanamgambo wa Al-Shabaab waliovamia gereza lenye ulinzi mkali lililojengwa chini ya ardhi katika jiji kuu la Mogadishu, alisema shahidi na serikali.

Eneo la Godka Jilaow, linalokaribia ikulu ya rais, linasheheni wapiganaji kadhaa wa kundi Al Shabaab, ambao wameshambulia vikali Somalia tangu 2007 na kupiga hatua muhimu mashinani mwaka huu.

“Tulisikia mlipuko mkubwa kwenye lango la gereza na punde si punde ufyatuaji risasi ukaanza,” mwanajeshi eneo hilo kwa jina Ahmed alieleza Reuters.

“Vikosi zaidi vilitumwa kumaliza wapiganaji. Operesheni bado inaendelea.”

Wakazi karibu eneo hilo vilevile walithibitisha mlipuko huo na milio ya risasi.

Al-Shabaab walikiri kuhusika na shambulizi.

“Tulilenga seli iliyojengwa chini ya ardhi inayolindwa na vikosi vya usalama. Kwanza ilianzia kwa gari la mlipuaji bomu wa kujitoa kafara kisha wapiganaji waliojihamu kwa silaha wakaingia uwanja wa seli na wanapigana ndani,” lilisema kundi hilo katika taarifa likisema wanajeshi ni miongoni mwa waliouawa na kujeruhiwa.

Kwenye taarifa ya televisheni iliyopeperushwa kupitia akaunti ya Facebook, serikali ilisema wapiganaji wa Shabaab walitumia gari lililobadilishwa kufanana na gari la vikosi vya usalama kupenya ndani.

“Baadhi ya wapiganaji walipigwa risasi. Kinachoendelea ni oparesheni ya mwisho kuangamiza wapiganaji walioshambulia eneo hilo,” ilisema.