Kiongozi wa wanamgambo Sudan apatikana na hatia ya uhalifu wa kivita
KIONGOZI wa wanamgambo wa Sudan amepatikana na hatia ya kufanya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika eneo la Darfur zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Ali Muhammad Ali Abd-Al-Rahman, anayejulikana pia kama Ali Kushayb, alikuwa mmoja wa viongozi wa Janjaweed, kundi linaloungwa mkono na serikali ambalo liliitikisa Darfur na kuua mamia ya maelfu ya watu.
Kushayb ni mtu wa kwanza kuhukumiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa ukatili Darfur.
Mzozo huo ulianza mwaka 2003 hadi 2020 na ulikuwa ni miongoni mwa maafa makubwa zaidi ya kibinadamu duniani, huku kukiwa na madai ya mauaji ya kikabila na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wasiokuwa Waarabu katika eneo hilo.
Miaka mitano baada ya kumalizika kwa mgogoro huo, Darfur imeendelea kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewen kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha RSF, ambacho asili yake ni Janjaweed.
Wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo, walionusurika walieleza jinsi vijiji vyao viliteketezwa, wanaume kuchinjwa na wanawake kulazimishwa kuwa watumwa wa ngono.
Jaji Joanna Korner alisema, “Mhusika alihimiza na kutoa maagizo ambayo yalisababisha mauaji, ubakaji na uharibifu uliofanywa na kundi la Janjaweed.”
Aliongeza kuwa Kushayb alitoa amri ya “kufuta na kufagia” makabila yasiyo ya Waarabu na kuwaagiza askari wasimwache mtu yeyote nyuma.
Kiongozi huyo wa wanamgambo alipatikana na hatia katika makosa 27, yakihusu mashambulio yaliyofanywa kati ya 2003 na 2004.
Waliohudhuria walisema kuwa wameridhika na hukumu huo.
Vita vya Darfur vilianza baada ya serikali iliyotawaliwa na Waarabu wakati huo kuwapa silaha kundi la Janjaweed, katika jaribio la kupambana na uasi kutoka makabila ya watu weusi wa Afrika.