Kiswahili kutumika katika shule na Vyuo Vikuu Somalia
SERIKALI ya Somalia imetangaza mpango wa kutumia Lugha ya Kiswahili katika shule na vyuo vikuu nchini humo kama hatua ya kuimarisha ushirikiano wake na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mamlaka ilisema lugha hiyo itapandishwa hadhi na kutumika shuleni kando na Kisomali, Kiarabu na Kiingereza.
Rais Hassan Sheikh Mohamud alivitaka vyuo vikuu vya Somalia kuikumbatia lugha ya Kiswahili kama msingi wa umoja na ushirikiano wa kikanda.
“Chuo Kikuu cha Taifa cha Somalia, pamoja na vyuo vikuu vyote vya Somalia, lazima viongoze katika kukuza Kiswahili, lugha muhimu katika eneo la Afrika Mashariki,” Rais Mohamud alisema.
Aliyasema hayo Jumanne katika ufunguzi wa Kongamano la pili la Ushirikiano wa Kiuchumi wa Afrika Mashariki (EACON 2025) katika mji mkuu, Mogadishu.
Waziri wa Elimu Farah Sheikh Abdulkadir alisema serikali inashirikiana na taasisi za kikanda kuandaa mfumo wa kufundisha Kiswahili nchi nzima.
“Tunajitahidi kuimarisha usomaji na matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Somalia. Tunataka kuona Kiswahili kinakuwa lugha ya mawasiliano, biashara na kujifunza, hata kuchukua nafasi ya Kiingereza wakati wa mkutano wetu ujao,” alisema.
Kiswahili, kinachozungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 kote Afrika Mashariki na Kati, tayari ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Toleo la mwaka huu la EACON lililenga kuimarisha ushirikiano, uzalishaji, biashara na uwekezaji katika kanda ya Afrika Mashariki.
Rais Mohamud alisema ushirikiano wa Somalia katika ukanda wa Afrika Mashariki tayari unachukua sura, unaakisiwa na kukua kwa uhusiano wa kiuchumi, biashara ya mipakani na kuongezeka kwa idadi ya wataalamu kutoka nchi jirani wanaochangia sekta ya umma na ya kibinafsi ya Somalia.
Alisisitiza kuwa awamu inayofuata ya ushirikiano huo lazima ipite zaidi ya biashara, akitoa wito wa ushirikiano wa kina wa kitamaduni na lugha ili kuimarisha utambulisho wa kikanda.
“Mogadishu daima imekuwa eneo la biashara na uhusiano. Kuandaa mkutano huu kunaonyesha dhamira ya Somalia katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kukuza amani, na kuendeleza ustawi wa pamoja wa Afrika Mashariki,” alisema.
Rais alitoa wito kwa wasomi, viongozi wa biashara, na watunga sera kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa kote katika umoja huo.