Gen-Z wakalia ngumu Rais Rajoelina wa Madagascar, washikilia ‘Must Go’
ANTANANARIVO, MADAGASCAR
RAIS wa Madagascar, Andry Rajoelina anaendelea kuandamwa na shinikizo za kuondoka madarakani huku Gen-Z Jumatano, Oktoba 8, 2025 wakikataa kushiriki mazungumzo ya kitaifa yaliyoitishwa naye na kumtaka abanduke madarakani.
Gen-Z walimpa kiongozi huyo makataa ya hadi jana ajiuzulu la sivyo wayageuze maandamano hayo kuwa mgomo na maasi makubwa katika taifa hilo.
Mnamo Jumatatu, Rajoelina alimtaja jenerali wa jeshi Ruphin Fortunat Zafisambo kama waziri mkuu, wiki moja baada ya kutimua baraza lake la mawaziri.
Kutimua baraza lake la mawaziri kulitokana na msukumo wa kusuluhisha masuala ambayo yalisababisha maandamano yaliyoanza Septemba 25.
Uteuzi huo hata hivyo haujanyoosha nyoyo za Gen-Z ambao mwanzoni waliingia barabarani kupinga ukosefu wa maji na kawi katika kisiwa hicho cha Bara Hindi chenye viwango vya juu vya umaskini.
“Lazima tuungane kupambana na maovu haya na kujenga jamii yenye msingi wa umoja, maelewano na heshima,” akasema Rajoelina.
“Kwa sababu hiyo, mazungumzo ya kitaifa na mashauriano hayo yatatoa jukwaa la kuwasikiliza raia na kusuluhisha changamoto zinazowakumba,” akasema Rajoelina.
Mazungumzo yaliyostahili kuandaliwa jana yakiratibiwa kuhudhuriwa na viongozi wa kidini, wanafunzi, wawakilishi wa vijana miongoni mwa wengine, hayakufanyika.
“Tunakataa kejeli hii ya mazungumzo na ualishi ambao rais ametuma. Hatutashiriki mazungumzo na serikali ambayo inawakandamiza raia wake, inawadhulumu na kuwapiga wakiandamana,” ikasema taarifa ya vuguvugu la Gen-Z ambalo limekuwa likiongoza maandamano hayo.
Mbali na kumtaka Rajoelina aondoke afisini, waandamanaji wamekuwa wakimtaka aombe msamaha kisha avunje Bunge la Seneti na Tume ya Uchaguzi.
Maandamano hayo yaliendelea Jumanne lakini yalitibuliwa na polisi na idadi ya waliojitokeza ilikuwa chini kuliko ya hapo awali.
Hiyo hiyo Jumanne, Rajoelina aliwateua mawaziri wapya wa Ulinzi na Usalama wa Kitaifa na kuwataka warejeshe taifa hilo katika mkondo wa usalama na amani.
“Msiwavumilie wale wanaowachochea watu,” akasema bila kutoa ufafanuzi zaidi.
Umoja wa Mataifa (UN) umesema kuwa zaidi ya watu 22 tayari wameaga kwenye maandamano hayo huku wengine 100 wakijeruhiwa. Serikali hata hivyo, imesema takwimu hizo ni za uongo.
Rajoelina yupo pabaya zaidi hasa baada ya waandamanaji kupinga na kukataa uteuzi wa waziri mkuu mpya.