• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
ODONGO: Ni aibu Gor kutumia jezi zilizotiwa viraka mechi za CAF

ODONGO: Ni aibu Gor kutumia jezi zilizotiwa viraka mechi za CAF

NA CECIL ODONGO

HATUA ya timu ya Gor Mahia kutumia jezi zilizotiwa viraka kuziba nembo ya kampuni ya bahati nasibu ya Sportpesa wakati wa mechi mbili za bara Afrika (CAF) inaibisha soka ya Kenya.

Gor Mahia ambao wanajivunia historia ya kupigiwa mfano ya soka walitumia jezi hizo wakati wa mechi ya kundi D ya Kombe la Mashirikisho (CAF) dhidi ya Zamalek nchini na Petro Atletico de Luanda nchini Angola.

Sababu ya K’Ogalo kuficha nembo ya wafadhili wao Sportpesa ni kwamba mdhamini wa mashindano ya CAF pia ni kampuni ya bahati nasibu kwa jina 1xBet, hali inayozua ushindani mkali katika matangazo ya kibiashara kwa manufaa ya kampuni hizo.

Hata hivyo jinsi wasemavyo Waswahili ‘Ukweli ingawa chungu niambie sinifiche’. Hapa K’Ogalo walichemsha na kutuletea aibu mbele ya timu zinazoshiriki kipute hicho.

Ingawa hivyo, kilichonishangaza zaidi ni kauli ya Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Omondi Aduda kwamba hawakuwa na fedha za kununua jezi nyingine na walipokea masharti hayo mechi ya kwanza ikinukia.

Bw Aduda alieleza kwamba wanakandarasi na kampuni ya kuwaletea jezi watawatengenezea jozi zima la mavazi hayo mwezi Aprili kulingana na mkataba wa kibiashara waliotia saini.

Ingawa naelewa alichoeleza Bw Aduda, sikubaliani naye kwamba hiyo ilikuwa sababu tosha ya klabu ya hadhi ya K’Ogalo kuvaa jezi za kuanika ‘umaskini wake’ nje na ndani ya nchi.

Vijisababu

Mashabiki wa Gor Mahia wanashindwa kuelewa kauli ya kila mara ya viongozi wa timu kwamba ‘hakuna pesa’. Jamani hata za kununua jezi za muda tu zilikosekana?

Ingawa hivyo, naomba wadau wa soka nchini, uongozi wa Gor na Waziri wa Michezo Rashid Echesa kutafuta njia ya kupata jezi za muda zisizotiwa viraka au rangi ya kuziba nembo ya Sportpesa ili timu hiyo izitumie kwenye mechi zilizosalia.

Hili linafaa kufanyika kabla ya mechi muhimu dhidi ya viongozi wa kundi D Na Hussein Dey kutoka Algeria Jumapili hii na ile ya marudiano ugenini Machi 3 kabla ya Zamalek ugenini Machi 10 kisha mchuano wa mwisho wa kundi hilo Machi 17 jijini Nairobi dhidi ya Petro Atletico de Luanda.

Iwapo K’Ogalo itafuzu kwa hatua ya mechi za robo fainali mwezi Aprili, natumai jezi zitakuwa tayari jinsi alivyoahidi Bw Aduda na hakutakuwa na la kuhofia.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali isiwaadhibu wazazi

MATHEKA: Heko kwa maafisa wetu wa polisi kwa kazi murua

adminleo