Macho kwa Kasait, Biwott wakiendea Sh3.4m Delhi Half Marathon
WAKENYA Lilian Kasait, Benard Biwott, Waethiopia Birhanu Legese na Alemaddis Eyayu watakuwa vivutio katika makala ya 20 ya Vedanta Delhi Half Marathon nchini India, Jumapili.
Bingwa mtetezi wa kinadada Eyayu atakabiliana na mshindi wa medali nyingi za mbio za nyika Kasait anayefunzwa na Mwitaliano Claudio Berardelli.
Kasait anatarajiwa kurejea kwa nguvu baada ya kushinda Prague Half Marathon. Analenga kuvunja rekodi ya Delhi Half ya wanawake ya dakika 1:04:46.
Eyayu aliyekamata nafasi ya tatu Berlin Half Marathon nchini Ujerumani mwezi Aprili, yuko tayari kutetea taji lake. Kwa wanaume, bingwa wa zamani wa Tokyo Marathon, Legese, atapimana ubabe na mshindi wa Paris Marathon, Biwott.
Wakenya wengine mjini Delhi ni Catherine Amang’ole, Grace Loibach, Usaac Kipkemboi, Alexa Matata, James Kipkogei, Susy Chemaimak na Monicah Wanjuhi.
Washindi watapokea Sh3.4 milioni. Kuna bonasi ya Sh1.5m kuweka rekodi.