Jinsi dawa ya kikohozi ilivyosababisha vifo vya watoto India
BAADHI ya wazazi huamini dawa ya kikohozi ni tiba ya haraka kwa mtoto anayekohoa usiku.
Lakini je, unajua kuwa dawa hiyo “isiyo na madhara” inaweza kuwa sumu hatari?
Wiki chache zilizopita, takriban watoto 19 walikufa nchini India baada ya kunywa dawa ya kikohozi yenye diethylene glycol, kiyeyusho hatari cha viwandani.
Dawa hiyo aina ya Coldrif iliundwa na kuuzwa nchini India Mamlaka ilimkamata anayemiliki kampuni iliyounda dawa hiyo.
Uchunguzi wa wataalamu wa afya ulibaini dawa hiyo ilikuwa na kemikali hatari ya viwandani, diethylene glycol, ambayo huharibu figo na kusababisha kifo ndani ya muda mfupi.
Mamlaka baadaye ilitangaza kuwa dawa zingine mbili za kikohozi, Respifresh TR na Relife, pia zina diethylene glycol.
Siyo mara ya kwanza kisa kama hicho kutokea. Katika majimbo mengine kama Rajasthan na Kashmir, watoto kadhaa wamepoteza maisha kwa sababu ya dawa hizo zenye sumu. Mwaka 2023, dawa za kikohozi kutoka India zilitajwa kusababisha vifo vya watoto 70 nchini Gambia na 18 nchini Uzbekistan.
Kinachosikitisha ni kuwa vifo hivi vimekuwa vikifanyika kila mwaka, licha ya serikali ya India kuahidi kuchukua hatua. Watengenezaji wa dawa hizo huendelea wanatumia bidhaa za bei nafuu bila kufanyiwa ukaguzi wa kutosha.

Lakini tatizo si India pekee. Hata hapa nyumbani Kenya, maduka mengi ya dawa bado huuza dawa za kikohozi zenye codeine bila ushauri wa daktari. Wengine huwauzia vijana wanaotaka kulewa kwa bei rahisi. Wataalamu wa afya wanasema uraibu huu unaweza kuharibu ubongo na figo, hasa miongoni mwa watoto wadogo.
Daktari wa watoto katika mojawapo wa hospitali nchini Moses Ouma, anasema wazazi wengi huamini dawa ni ishara ya matibabu.
“Watoto wengi hupewa dawa kila wanapokohoa, ilhali kikohozi ni dalili ya mwili kupambana na maambukizi. Mzazi anafaa kuwa makini sana kabla ya kununua na kumpa mwanawe dawa,” anasema Dkt. Ouma.
Wizara ya Afya India tayari imeanzisha uchunguzi na kupiga marufuku baadhi ya dawa hizo, lakini wataalamu wanasema mfumo wa udhibiti ni dhaifu. Soko la dawa za kikohozi nchini humo linatarajiwa kufikia mabilioni ifikapo mwaka 2035, jambo linaloonesha kuwa biashara hii bado inakua licha ya vifo.
Kwa wataalamu wa afya, suluhisho ni kuwahamasisha wazazi na udhibiti mkali wa dawa sokoni.
“Wazazi wanapaswa kumwona daktari kabla ya kumpa mtoto dawa yoyote. Kikohozi cha kawaida hupotea baada ya siku chache,” anasema Dkt. Ouma.