Uchu wa “TUTAM” unavyomsukuma Rais Ruto kuchukua viongozi wa upinzani
RAIS William Ruto anaonekana kuendelea kulemaza upinzani kwa kuvutia upande wake viongozi wa mrengo huo kwa kisingizio cha kupalilia umoja wa kitaifa.
Hatua hiyo inaonekana kukiuka mapendekezo ya ripoti ya kamati ya mazungumzo ya kitaifa (NADCO) kuheshimiwa kwa uhuru wa vyama vya kisiasa.
Aidha, hatua hii ni kinyume cha Katiba na Sheria ya Vyama vya Kisiasa zinazolinda uhuru wa vyama vya kisiasa.
Kabla ya kukiri Ijumaa kwamba ndiye alimshawishi mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi kujiondoa kutoka kinyang’anyiro cha useneta wa Baringo Novemba 27, 2025, Rais Ruto alikuwa katika Ikulu ya Nairobi akimpokea rasmi Mbunge Magharibi Charles Ngusya Nguna wa chama cha Wiper “kwa kukubali kufanyakazi na mrengo wa serikali jumuishi.”
“Haswa, namshukuru Mbunge wa Mwingi Magharibi Charles Ngusya Nguna kwa kumua kujiunga na upande wake ili kufanikisha ajenda ya maendeleo katika eneo bunge lake,” rais akasema alipowahutubia viongozi wa Ukambani waliomtembelea katika Ikulu kujadili maandalizi ya sherehe za kitaifa za Mashujaa Dei zitakazofanyika mjini Kitui Oktoba 20,2025
Uhusiano wa Bw Nguna na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ulianza kudhoofika kuanzia Oktoba mwaka jana alipokaidi msimamo wa chama hicho na kuunga mkono hoja ya kumtimua aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Saa chache baada ya kumnasa rasmi Bw Nguna, Dkt Ruto alifululuza hadi Kabarak, nyumbani mwa Gideon kwa mkutano na viongozi wa mashinani wa Kanu.
“Mimi ndiye nilimtafuta Gideon kwa sababu uwiano wa kitaifa ni muhimu zaidi kuliko tofautia zetu. Hii ni sehemu ya mpango wangu wa kuleta maridhiano ya kisiasa nchini Kenya ili sote kama viongozi tusaidiane kusukuma gurudumu la maendeleo kwa manufaa ya watu wetu,” akafichua huku akirejelea mazungumzo yake na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na ushirikiano wake na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Awali, Jumatano, seneta huyo wa zamani alikutana na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi na saa chache baadaye Gideon anajiondoa katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Baringo, kumpisha mgombeaji wa UDA Vincent Chemitei. Kiti hicho kilisalia wazi mnamo Aprili 30, 2025 kufuatia kifo cha Seneta William Cheptumo.
Isitoshe, mnamo Septemba Rais Ruto alilemaza mpango wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) wa kujikuza nje ya ngome yake ya Mlima Kenya, alipomshawishi mgombeaji wake katika uchaguzi mdogo katika eneo bunge la Banissa kujiondoa.
Adan Mohamed almaarufu “Kiongozi” ambaye alikuwa ametawazwa kuwa mpeperusha bendera wa chama hicho, kinachoongozwa na Bw Gachagua, alikiri kuwa kujiondoa kwake kulichangiwa na “presha” kutoka kwa Rais Ruto.
Mwanasiasa huyo alikutana na Rais katika Ikulu ya Nairobi mnamo Septemba 17 akiandamana na Gavana wa Mandera Mohamed Adan Khalif na Seneta Ali Roba.
Bw Mohamed, ambaye aliwania kiti Banissa katika uchaguzi mkuu wa 2022 kwa tiketi ya ODM na kuwa wa pili kwa kura 7,775, alitangaza kwamba atamuunga mkono mgombeaji wa UDA Ahmed Maalim Hassan almaarufu Barre.
Kiti hicho cha ubunge kilisalia wazi kufuatia kifo cha mbunge Kallow Maalim Hassan mnamo Machi 23, 2023 katika ajali mtaani South C, Nairobi.
Marehemu Hassan alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha United Democratic Movement (UDM) kwa kuzoa jumla ya kura 13, 659.
Kulingana na mchangamuzi wa masuala ya kisiasa Gitile Naituli, nia ya Rais Ruto ni kujiongezea ushawishi wa kisiasa kwa manufaa katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“Naam, Rais Ruto haheshimu Katiba na sheria ya vyama vya kisiasa zinazolinda uhuru wa vyama vya kisiasa. Lengo lake kuu ni kujiweka katika nafasi bora ya kushinda tena katika uchaguzi mkuu ujao,” anaeleza.