Vita vya ubabe vyatisha mrengo wa upinzani
MKUTANO wa faragha kati ya Waziri wa zamani Fred Matiang’i, kiongozi wa Party of National Unity (PNU) Peter Munya na naibu kiongozi wa chama cha DAP-K George Natembeya umeibua tetesi kuhusa uwezekana wa wao kuunda mrengo mwingine wa kisiasa kuelekea 2027.
Watatu hao walikutana Jumatano Oktoba 8, katika mkahawa mmoja kaunti ya Kiambu wadadisi wakisema hiyo ni hatua ya kwanza ya wao kusuka vuguvugu jingine la kisiasa kuendeleza ajenda ya kumwondoa mamlakani Rais William Ruto.
“Bila shaka sio kawaida kwa wanasiasa kukutana kisadfa. Yao huwa ni mikutano ya kimkakati; iliyopangwa na yenye ajenda mahsusi ya kisiasa,” anasema Herman Manyora.
“Kwa hivyo, kuna kuna uwezekano kwamba Matiang’i, Munya na Natembeya walikuwa wakijiandaa kuunda vuguvugu jingine la kisiasa nje ya Umoja wa Upinzani, ambao tayari unaonekana kuwa u tayari kumwidhinisha Kalonzo Musyoka kuwa mpeperusha bendera wake katika uchaguzi wa urais 2027,” anaongeza.
Kulingana na Manyora, Dkt Matiang’i, amewaleta Mbw Munya na Natembeya upande wake katika jitihada za kujipatia sura na nguvu ya kitaifa baada ya azma yake kupata “baraka” za chama cha Jubilee chake Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
“Labda hii ni sehemu za mpango wa Dkt Matiang’i kupanua mawanda yake nje ya ng’ome yake ya eneo la Gusii. Anataka kutumia Natembeya kuitia guu ndani ya jamii ya Waluhya huku akimtumia Munya kupenya Meru. Hii ni siasa,” anaeleza mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Nairobi.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa ODM, kaunti ya Nairobi George Aladwa (na Mbunge wa Makadara) anayeunga mkono serikali jumuishi inayoongozwa na Rais William Ruto, anataja mkutano kiashirio kwamba Dkt Matiang’i anapania kujitenga na mrengo wa upinzani unaoongwa na Rigathi Gachagua na Kalonzo Musyoka.
“Inaonekana kuwa huyu Matiang’i anataka kujitenga kwa sababu ni wazi kwamba lile kundi la Gachagua halimtaki kwa sababu anaungwa mkono na Uhuru,” anaongeza.
Lakini Ijumaa, Matiang’i aliungana na vinara wengine wa upinzani katika bustani ya Uhuru kwa kongamano la wajumbe wa chama cha Wiper Patriotic Front (WPF).
Bw Gachagua na wandani wake wamekuwa wakimshambulia Dkt Matiang’i kwa maneno tangu alipoonyesha nia ya kuwania urais kwa tiketi ya Jubilee. Wanahisi kuwa hatua hiyo itayeyusha ushawishi wa Bw Gachagua katika eneo la Mlima Kenya, ambako ndiko Jubilee inao idadi kubwa ya wafuasi.
Hata hivyo, Dkt Matiang’i amepuuzilia mbali madai kwamba mkutano huo ulikuwa na ajenda zake kisiasa akisema walikutana kumpa pole Bw Munya kufuatia kifo cha nyanyake na wala haukuwa wa kupanga mikakati ya kisiasa.
“Asubuhi hii, mimi na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya tulikutana na Waziri wa zamani Peter Munya kumpa pole zetu kufuati kifo cha nyanyake mpendwa Mama Mwakairu Rukunga (Bamung’o),” akasema kwenye taarifa saa kadhaa baada ya mkutano huo.
Lakini kulingana na Bw Dismus Mokua, ni kawaida kwa wanasiasa kutumia mikutano kama hiyo ya “kupeana pole” kupanga mikakati ya kisiasa.
“Ni kweli kwamba Bw Munya amefiwa na ni jambo la kawaida kwa marafikize kumpa pole. Lakini swali ni je, mbona Matiang’i akaandamana na Gavana Natembeya pekee anapokutana naye kumpa pole? Mbona hakuandamana na vinara wa upinzani kama vile Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Martha Karua na wengine?” akauliza.
“Huenda wanasiasa hao walikutanishwa na ajenda nyingine, mbali na kuomboleza kutoa pole zao kwa Bw Munya kufuatia kifo cha nyanya. Ikiwa wanasiasa huchapa siasa katika hafla za mazishi, sembuse mkutano wa kumfariji mwenzao aliyefiwa,” Bw Mokua anaongeza.
Dkt Matiang’i na Mbw Munya na Natembeya wamewahi kufanya kazi pamoja katika serikali ya iliyopita ya Bw Kenyatta. Dkt Matiang’i alipohudumu kama Waziri wa Usalama, Bw Natembeya alikuwa mdogo wake akihudumu kama Mshirikishi wa Ukanda wa Bonde la Ufa.
Naye Bw Munya alihudumu kama Waziri wa Kilimo katika serikali hiyo Bw Kenyatta.
Kwa hivyo, kulingana na Bw Mokua, ni rahisi kwa Mbw Munya na Natembeya kushirikiana na Bw Matiang’i kisiasa.