Presha kwa mawaziri serikali ikilenga ushindi katika chaguzi ndogo
RAIS William Ruto alipowateua mawaziri wapya kuingia katika serikali jumuishi, matarajio yalikuwa kwamba wangesaidia kuendesha serikali yake pamoja na masuala ya kitaifa.
Hata hivyo, ukweli wa mambo ni kwamba uteuzi huo ulikuwa na malengo ya kisiasa – hasa kuwaingiza wandani wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Na sasa mawaziri hao wanakumbwa na wakati mgumu katika chaguzi ndogo zijazo kudhihirisha mchango wao wa kisiasa huku wakipigia debe wagombeaji wanaoungwa mkono na serikali jumuishi.
Licha ya agizo la Mahakama Kuu mwezi Juni, maafisa wa serikali wamekuwa wakifanya kampeni za wazi kumpiga jeki Rais Ruto na wagombeaji wengine, kinyume na maagizo ya mahakama kwamba kampeni za mapema nje ya kipindi rasmi cha uchaguzi zinakiuka usawa na haki ya uchaguzi wa wazi na huru.
Ingawa mawaziri hao wana wizara zao maalum za kutekeleza sera za serikali, wamekuwa wakishinikizwa kusaidia Rais Ruto kupata awamu ya pili huku pia wakishawishi siasa mashinani ili serikali jumuishi isikose imani kwa umma.
Wachambuzi wa kisiasa wanasema chaguzi ndogo zilizopangwa kufanyika Novemba 27 zitakuwa jaribio la uwezo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), na pia fursa kwa mawaziri wapya kuonyesha uaminifu wao kwa Bw Odinga na Rais Ruto.
Mbinu zote za kisiasa zinatumiwa, kutoka kwa matumizi ya fedha kuwashawishi wapiga kura hadi kushawishi wagombeaji wengine wajiondoe kwa niaba ya wale wanaoungwa mkono na serikali.
Katika chaguzi hizo, maeneo muhimu ni pamoja na useneta wa Baringo na ubunge katika maeneo ya Magarini, Malava, Ugunja, Kasipul, Banisa, na Mbeere Kaskazini.
Waziri wa Kawi na Petroli, Bw Opiyo Wandayi, alitangaza kumuunga mkono Moses Omondi wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Ugunja, akisema ni mgombeaji wa serikali jumuishi, akisisitiza kuwa bado yuko ndani ya chama cha Orange (ODM) licha ya kuwa waziri.
Wagombeaji wengine waliopitishwa na IEBC ni pamoja na Erick Ofiro (Jubilee), Vincent Olengo ( anayeegemea vuguvugu la Kenya Moja), Fredrick Ochiel (UDM), Benson Obol (United Green Movement), Chrispine Oduor (KANU), Dkt Maurice Okumu (Federal Party), Orodi Odhiambo (Wiper) na Oliver Ochieng (Nation Liberal Party).
Wandayi alisihi wakazi wa Ugunja wasimuangushe, akisisitiza kuwa ushindi wa kishindo utampa heshima kitaifa. Rais Ruto na Bw Odinga wamekubaliana kuwasimamisha wagombeaji wa pamoja katika maeneo ya Kasipul, Ugunja na Malava ili kuepuka kugawanya kura.
Katika Kasipul, ODM inawakilishwa na Boyd Were anayekabiliana na wagombeaji huru Aroko Philip na Bior Robert. Homa Bay, nyumbani kwa Waziri wa Fedha John Mbadi, imegeuka kuwa uwanja muhimu kwa ODM kutetea nafasi hiyo.
Malava imegeuka kuwa mtihani kwa Musalia Mudavadi (Waziri Mkuu) ambaye anampigia debe David Ndakwa (UDA), anayekabiliana na Seth Panyako (DAP-K). Wagombeaji wengine ni Wilberforce Tuvai (Kenya Moja), James Angatia (ARC), na Edgar Busiega (DCP ya Gachagua).
Katika Mbeere Kaskazini, kiti hicho kiliachwa wazi baada ya Bw Geoffrey Ruku kuteuliwa kuwa waziri. Amekuwa akimpigia debe Leonard Muthende (UDA) huku akishutumiwa na Justin Muturi kwa kutumia rasilmali za serikali kisiasa.
Muthende anamenyana na Newton Kariuki (DP), Duncan Mbui (Chama Cha Kazi), na wengine sita. Naibu rais Prof Kithure Kindiki anatumai ushindi wa mgombeaji wao utathibitisha ushawishi wake eneo la Mlima Kenya Mashariki.
Katika Magarini, Harrison Kombe wa ODM ni mgombeaji wa serikali Jumuishi baada ya UDA kumuunga mkono ili kushinda kiti hicho. Hii inatoa shinikizo kwa mawaziri wanaotoka Pwani Hassan Joho na Salim Mvurya kuonyesha ushawishi na mchango wao kisiasa katika serikal.