Kimataifa

Biden aendelea kupokea matibabu ya saratani

Na MASHIRIKA October 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WASHINGTON DC, AMERIKA

ALIYEKUWA rais Joe Biden anapokea tiba ya mionzi kama sehemu ya matibabu yake ya saratani ya tezi dume, kwa mujibu wa msemaji wake.

Msemaji wake vilevile alisema Biden, 82, anapokea matibabu ya homoni, pasipo kutoa maelezo ya kina.

Tiba ya mionzi ilitarajiwa kuchukua wiki tano na iliashiria awamu mpya katika utunzaji wake, duru zilieleza shirika la habari la NBC.

Mei, afisi ya Biden ilitangaza kuwa amepatikana na aina sugu ya gonjwa hilo, lililokuwa limesambaa mifupani mwake.

Ugunduzi huo ulijiri baada ya mwanasiasa huyo wa Democratic kuripoti dalili kwenye mkondo wake wa mkojo zilizoelekeza madaktari kupata kijifundo kwenye tezi dume zake.

Afisi ya Biden ilisema wakati huo kwamba “alipatikana kuugua saratani ya tezi dume zilizosheheni Gleason daraja la 9 (Gredi Kundi 5) iliyoenea kwenye mifupa.”

“Ingawa hii inaashiria aina sugu ya gonjwa hilo, saratani inaonekana kutulizwa na homoni, jambo linalowezesha kuidhibiti kwa njia bora zaidi.”

Daraja tisa la Gleason lilimaanisha ugonjwa wake uliorodheshwa kama “kiwango cha juu” na seli za saratani zingeenea kwa kasi, kulingana na taasisi ya Utafiti wa Saratani Uingereza.