Kimataifa

Hakuna ‘Must Go’: Biya, 92, aenda debeni akitarajiwa kujinyakulia muhula wa 8 Cameroon

Na CHARLES WASONGA, REUTERS October 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

YOUNDE, CAMEROON

RAIA walipiga kura Jumapili, Oktoba 12, 2025 katika uchaguzi wa urais ambapo rais wa sasa, Paul Biya, 92, kiongozi mkongwe zaidi duniani, anatarajiwa pakubwa kudumisha utawala wake wa miaka 43 licha ya upinzani unaoshinikiza vikali kuwepo mabadiliko.

Upinzani uliogawanyika unaoshirikisha wagombeaji 11 unakabiliana na Biya ambaye licha ya umri wake mpevu na kudhoofika kiafya, amepuuzilia mbali wito wa kustaafu na kuwania muhula wake wa nane mamlakani.

“Mgombea wetu ni mzima kama kigongo…na ana uwezo wa kuendeleza alichoanzisha,” waziri wa leba na katibu mkuu wa chama tawala, Grégoire Owona, alieleza redio ya Ufaransa RFI Septemba.

Sehemu kubwa ya raia 7.8 milioni hawawezi kukumbuka kiongozi mwingine yeyote isipokuwa Biya ambaye ameshikilia urais kimabavu tangu 1982.

Kura inafanyika kukiwa na hali ya kudumaa kisiasa, kero la gharama ya juu ya maisha na misukosuko kijamii.

Upinzani umeshutumu tume ya uchaguzi nchini kwa kunyenyekea chama tawala na mpinzani mwenye ushawishi Maurice Kamto, amezuiwa kuwania na korti.

Wagombeaji wengine wanajumuisha mawaziri wa zamani Issa Tchiroma Bakary, aliyegura majuzi kambi ya rais, ambaye amekusanya maelfu ya watu katika mikutano kote nchini, na Bello Bouba Maigari, aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza kuteuliwa na Biya 1982.

Waangalizi wamesema kampeni zao mtawalia zilikosa ushikamano unaohitajika kukabili vilivyo utawala wa muda mrefu wa Biya.

Cameroon inakabiliwa na changamoto sugu kijamii na kiuchumi; thuluthi ya raia nchini wanaishi chini ya Sh257.44 kwa siku, ukosefu wa ajira kwa vijana umekithiri, na vijana wengi wameelezea kukatizwa tamaa na mchakato wa uchaguzi, wakitaja kukosa nafasi za uwakilishaji kiuchumi na kisiasa.