Stanley Kenga aamini Magarini ni kivumbi kati ya raia na serikali
UCHAGUZI mdogo wa Magarini utakuwa si tu uchaguzi wa kawaida kwani ubabe wa viongozi na wapigakura unatarajiwa kujitokeza.
Kuidhinishwa kwa Bw Stanley Kenga na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) kugombea kiti hicho kwa tiketi ya DCP; chama kinachoongozwa na aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua baada ya kuhama chama cha UDA kunatarajiwa kutifua kivumbi dhidi ya viongozi walioko mamlakani dhidi ya wakazi.
Vyama vikuu nchini ODM, UDA na chama cha Spika wa Seneti Amason Kingi cha PAA vinatarajiwa kupigia debe aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Harrison Kombe wa ODM huku Bw Kenga naye akionya kuwa yatakuwa ni mapambano ya wakazi dhidi ya viongozi.
Bw Kenga alijiunga na DCP baada ya kudinda kushurutishwa kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho kupitia chama cha UDA.
Bw Kenga alisema hatajutia kamwe uamuzi wake kuingia Chama cha DCP na kumpa nafasi ya kugombea ubunge wa Magarini, akisema wakazi wa Magarini wako na nafasi nyingine katika uchaguzi huo mdogo.
“Wakati milango ilipofungwa ile ng’ambo ya pili hapa DCP, mlitufungulia milango, mkatupokea na tunashukuru. Ninasema kwamba tuko tayari na tutachukua kiti cha Magarini kupitia DCP kwani kura tunazo na ziko kwa wananchi. Ninawarai wafausi wangu kutorudi nyuma katika kupigania demokrasia,” alisema Kenga.
Baadhi ya wakazi wanasema Bw Kenga anastahili kuwa kwenye debe kwani ameng’ang’ana mahakamani miaka mwili hivyo basi anafaa kupata haki yake.
“Ana kibarua kigumu kwani Rais William Ruto, Kinara wa ODM Raila Odinga na Bw Kingi wataleta nguvu zote kusaidia Bw Kombe ambaye wanamuunga mkono. Kupoteza kwa Kombe kutakuwa aibu kubwa kwa viongozi hao lakini Bw Kenga ana nguvu ya wapigakura,” asema Bw Maalimu Mabruk, mkazi wa Magarini.
Licha ya wagombeaji 10 kuidhinishwa na IEBC kwa uchaguzi mdogo huo wa tarehe 27 Novemba, kinyang’anyiro kikuu cha Magarini kinatarajiwa kuwa cha farasi wawili (Bw Kombe na Bw Kenga) ambao wamekuwa mahasimu tangu uchaguzi mkuu wa 2022.
Wengine ambao wameidhinishwa ni Samuel Kombe Nzai wa chama cha Wiper, Furaha Ngumbao Chengo wa chama cha DNA, Hamadi Karisa Chadi (Roots Party), Emmanuel Kitsao Kalama (TWAP) na John Sulubu Masha wa chama cha Kenya Social Congress.
Hata hivyo, mgombea wa kiti hicho kupitia chama cha Federal Party of Kenya Jacob Themo Kwicha alikosa kuidhinishwa na IEBC baada ya cheti chake kutoka kwa chama kuonyesha kwamba anawania kiti cha uwakilishi wadi.
Mwezi wa Agosti 2022, Bw Kombe wa ODM alitangazwa mshindi kwa ushindi finyu wa kura 22 dhidi ya mgombeaji wa UDA Bw Kenga.
Kutokana na madai ya Bw Kombe kujiongezea kura kwenye masanduku ya kupigia kura, Bw Kenga alielekea mahakamani na mwezi wa tatu 2024, uchaguzi huo ulifitiliwa mbali hivyo basi kusababisha kutanganzwa kwa kiti hicho kuwa wazi na kusababisha uchaguzi mdogo.
Hata hivyo, IEBC ilichukua zaidi ya miezi 18 kutangaza uchaguzi huo mdogo jambo ambalo limeghadhabisha wakazi kwani wamekaa muda mrefu bila kuwa na mwakilishi mbungeni kinyume na Katiba.
Kucheleweshwa kwa kesi ya Magarini kumeenda kinyume na Sheria za Uchaguzi kifungu cha 75 ambacho kimeweka miezi sita kutatua mzozo wa kesi za Uchaguzi katika mahakama kuu na siku 90 katika mahakama ya rufaa kisha ile ya upeo kutatua kesi husika.