Habari

UCHUMI: Uganda yapaa Kenya ikichechemea

February 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na BENSON MATHEKA

Kwa Muhtasari:

  • Wakenya wanaendelea kununua bidhaa kwa wingi kutoka Uganda badala ya kununua zinazotengenezewa humu nchini
  • Bidhaa kutoka Uganda zinazoagizwa na Wakenya ni mayai, maziwa, sukari na maharagwe
  • Kwa sababu ya mazingira bora ya kibiashara, kampuni zilizokuwa na makao Nairobi zimehamia Kampala
  • Haya yote yametokana na serikali ya Kenya kuongeza ushuru wa bidhaa za humu nchini na zile za kutoka nje ya nchi

KENYA imo hatarini kupoteza nafasi yake kama simba wa uchumi Afrika Mashariki baada ya mataifa jirani hasa Uganda kufanikiwa kuuza bidhaa zaidi nyingi hapa nchini kuliko inazonunua.

Hii inamaanisha kudidimia kwa viwanda vya Kenya, watu zaidi kupoteza nafasi za kazi na kupotea kwa ushuru.

Ingawa Rais Museveni anasema Uganda imefanikiwa kuafikia haya kutokana na amani iliyoletwa na jeshi la nchi hiyo, wadadisi wanasema mazingara bora ya kiuchumi nchini humo ndiyo yamechangia hali hiyo.

Takwimu zinaonyesha kuwa Wakenya wanaendelea kununua bidhaa kwa wingi kutoka mataifa jirani hasa Uganda na Tanzania badala ya kununua zinazotengenezewa nchini au zinazoigizwa nchini moja kwa moja kutoka ng’ambo kama vile India na China.

Margaret Wanjiru anasema kwamba huwa anaenda Uganda kununua nguo anazouza Nairobi kwa sababu ya bei nafuu: “Huwa ninaenda Kampala mara tatu kwa wiki kununua nguo ambazo hapa Kenya ni ghali mno. Tangu nianze miaka mitatu nimekuwa nikipata faida kubwa kuliko mbeleni,” asema Bi Wanjiru.

Kwa kipindi cha miaka minne sasa, Uganda, ambayo haina bandari kama Kenya, imekuwa ikiuzia Kenya bidhaa za mabilioni ya pesa kuliko inazonunua hapa nchini.

Bidhaa hizo ni pamoja na zinazotoka ndani ya uchumi wa Uganda kama vile mayai, maziwa, sukari na maharagwe. Pia wafanyibiashara wa Kenya wanasafiri Uganda kununua nguo, bidhaa za urembo, mbao na vipuri vya magari kwa ajili ya kuziuza nchini.

Kulingana na mtaalamu wa uchumi, Robert Kamande, Uganda imefanikiwa kuuzia Kenya bidhaa za kilimo kutokana na mfumo bora wa kusaidia wakulima na kupunguzwa kwa ushuru wa fatailaiza, mbegu na pembejeo. Hii ni kinyume na Kenya ambapo gharama za kilimo ziko juu.

Gharama ya chini ya uzalishaji 

“Ndio maana maziwa yanayotoka Uganda yanauzwa Sh40 kwa pakiti ilihali ya Kenya ni Sh50. Hii inamaanisha gharama za uzalishaji Uganda ni nafuu sana ukizingatia kuwa wanauza Sh40 wakiwa wameweka gharama za usafiri,” asema Bw Kamande.

Mwaka 2018, takwimu za Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) zilionyesha kuwa Uganda iliendelea kuuzia Kenya bidhaa nyingi zaidi, tofauti na awali ilipokuwa ikinunua bidhaa hizo kutoka Kenya.

“Kwa sababu ya mazingira bora ya kibiashara, kampuni zilizokuwa na makao Nairobi zimehamia Kampala. Na kwa sababu ya hali nafuu ya kibiashara na ushuru, gharama ya kutengeneza bidhaa huwa ya chini Uganda, na hivyo basi kuvutia wafanyabiashara wa humu nchini,” aeleza mtaalamu wa biashara Robert Kamande.

Takwimu za KRA zinaonyesha kuwa bidhaa ambazo Kenya huuzia Uganda zimekuwa zikipungua kwa kiwango kikubwa tangu 2015.

Wafanyabiashara kutoka Kenya wanachagua kusafiri hadi Uganda kununua bidhaa kwa bei nafuu kuliko kuziagiza moja kwa moja kutoka China au kuzinunua nchini ambako zinauzwa kwa bei ghali baada ya serikali kuongeza ushuru.

Uganda inavyokwepa bandari

Ili kurahisisha biashara, wafanyabiashara wa Uganda wamekuwa wakisafirisha bidhaa kwa ndege moja kwa moja kutoka China hadi Kampala badala ya kuzipitishia bandari ya Mombasa ambapo zinatozwa ushuru mkubwa kabla ya kuzisafirisha kwa reli na matrela hadi Uganda.

Kulingana na Bw Kamande, baadhi ya bidhaa inazoagiza kutoka China huwa pia zinatengenezewa nchini lakini wafanyabiashara huamua kuzinunua Kampala kwa sababu ya bei nafuu.

“Uganda haiwalimbikizii wafanyabiashara mzigo wa kodi kama Kenya. Masharti ya biashara ni nafuu na ndiyo sababu hata magari na vipuri vya magari ni bei nafuu kuliko Kenya,” aeleza Bw Kamande.

Bali na magari, Wakenya wamekuwa wakinunua nguo, bidhaa za urembo, maziwa na mayai kutoka Uganda, jambo ambalo wadadisi wanasema ni tisho kwa uchumi wa nchi kwa sababu kununua bidhaa hizi kutoka nchi jirani ni kuua viwanda vya humu nchini na kunyima Wakenya nafasi za kazi.

Ingawa Kenya ina viwanda vikubwa vya bidhaa za chuma Afrika Mashariki na Kati, Wakenya wamekuwa wakinunua bidhaa hizi kutoka Uganda kufuatia ushuru wa asilimia 35 uliowekwa na serikali kwenye bajeti ya 2018/2019.

Kwenye bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Herny Rotich aliweka ushuru wa asilimia 35 kwa mavazi na viatu kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda viwanda vya humu nchini.

Sekta ya samani iliuawa

“Kwa sababu ya ushuru mpya wa bidhaa za mbao, serikali iliua kampuni kadhaa zilizokuwa zikihusika na fanicha na baadhi zikahamia Uganda na kuacha maelfu ya Wakenya bila kazi,” asema Bw Raju Shah, ambaye alifunga kampuni yake nchini mwaka jana.

Anasema baada ya serikali kuchukua hatua hii ikisema ililenga kulinda viwanda vya humu nchini, bidhaa hizo zinaendelea kuingia Kenya kutoka Uganda kwa bei nafuu zaidi.

Wadadisi wanasema baada ya Kenya kuongeza ushuru wa bidhaa kutoka nje ya nchi, Uganda iliwafungulia milango wawekezaji wa Kenya kwa kupunguza kodi.

“Matokeo yamekuwa ni kuongezeka kwa bidhaa zinazouzwa nchini kutoka mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa Uganda na Tanzania,” asema Bw Kamande.