Habari za Kitaifa

Raila ni wa kumi kufanyiwa mazishi ya kitaifa Kenya

Na Steve Otieno October 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAZISHI ya kitaifa nchini Kenya huwa ni sherehe ya kipekee, kwa watu waliotoa mchango mkubwa kwa taifa. Hadi kufikia mazishi ya Raila Odinga mwaka 2025, Kenya ilikuwa imeshuhudia mazishi kumi ya kitaifa, kila moja likiwa na uzito wake wa kihistoria, kisiasa au kitaifa.

Mazishi ya kwanza ya kitaifa yalikuwa ya Mzee Jomo Kenyatta mwaka 1978. Mwili wake uliwekwa katika majengo ya Bunge kwa siku 10, na alipumzishwa kwa heshima kamili za kijeshi, ikiwemo saluti ya mizinga 19 na ndege za kijeshi kupaa angani.

Baada ya miaka 25, Kenya ilifanya mazishi ya kitaifa ya pili kwa Makamu wa Rais Michael Kijana Wamalwa mwaka 2003. Ingawa yalikuwa ya serikali, hayakuwa na heshima zote za kijeshi.

Mazishi ya kitaifa ya tatu yalikuwa ya mshindi wa Tuzo ya Nobel Profesa Wangari Maathai mwaka 2011. Mwili wake ulifunikwa kwa jeneza lililotengenezwa kwa mianzi, kwa heshima ya mazingira aliyotetea.

Mazishi ya nne yalikuwa ya Lucy Kibaki, mke wa Rais mstaafu Mwai Kibaki, mwaka 2016 na ya tano yalifanyika mwaka 2020 baada ya kifo cha Rais mstaafu Daniel arap Moi. Alipatiwa heshima kamili za kijeshi kama alivyopata Kenyatta.

Mazishi ya sita yalikuwa ya Rais mstaafu Mwai Kibaki mwaka 2022. Alizikwa kwa saluti 19 na msafara wa kijeshi.

Mazishi ya saba yalikuwa ya Mukami Kimathi mwaka 2023, mjane wa Dedan Kimathi na nane yalikuwa ya Kelvin Kiptum, bingwa wa mbio, mwaka huo huo. Mazishi ya tisa yalikuwa ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Francis Ogolla mwaka 2024.

Mazishi ya kumi ni ya Raila Odinga mwaka 2025 — kiongozi wa upinzani, mtetezi wa demokrasia na “rais ambaye Kenya haikuwahi kuwa naye rasmi.”