Raila aacha pengo Kenya na Afrika
KIFO cha Raila Amolo Odinga kimeacha pengo kubwa kujaza si tu katika siasa za Kenya, bali pia katika historia pana ya bara la Afrika.
Viongozi wa utawala, kisiasa na wachanganuzi wa siasa wanakubaliana kuwa Raila alikuwa zaidi ya mwanasiasa, alikuwa sauti ya matumaini, nembo ya mapambano, na alama ya uthubutu wa kweli katika kizazi chake.
Kwa miongo kadhaa, Raila alisimama kidete kama mtetezi wa demokrasia, haki za binadamu, na utawala wa sheria. Katika misingi hii, alikumbatia maumivu, akavumilia mateso, na hata kufungwa jela kwa miaka mingi kuliko kiongozi mwingine yeyote wa upinzani katika Kenya huru – yote kwa ajili ya taifa alilolipenda kwa dhati.
“Raila hakuwa mwanasiasa wa kawaida. Alijitokeza kama nguzo kuu ya upinzani dhidi ya tawala dhalimu, akichochea mageuzi ambayo hatimaye yalizaa Katiba ya 2010 – mojawapo ya mafanikio makubwa zaidi ya kisiasa nchini Kenya. Ujasiri wake ulimletea majina mengi ya heshima kutoka kwa wananchi na viongozi wa kimataifa,” asema mchanganuzi wa siasa James Obwaka.
Wengi walimwita ‘Baba wa Demokrasia ya Kisasa Kenya’, huku wengine wakimuita ‘Tinga’ – jina lililoashiria nguvu na msimamo wake usiyoyumbayumba. Wafuasi wake waaminifu walimuita kwa upendo “Jakom” na “Agwambo” majina la kijaluo yanayomaanisha mtu mwenye uwezo wa ajabu au wa kipekee.
Kwa Wakenya, Raila alikuwa mfano wa uthabiti – mtu ambaye hakuchoka kudai haki, hata alipokataliwa, kudhulumiwa, au kunyamazishwa. Aliitisha maandamano na kuingia barabarani kuyaongoza, na mara kadhaa alikubali kuwa kiongozi wa upinzani kwa heshima bila kushiriki katika mifumo aliyohisi haikuwa ya haki.
Katika uhai wake, Raila alifichua kashfa nyingi kubwa zilizotikisa serikali na alisimama kidete kuhoji matumizi ya fedha za umma.
Msimamo wake dhidi ya ufisadi ulimweka kwenye mgongano na watawala, lakini pia ulimfanya kuwa shujaa wa umma.
Alijulikana kwa kutoa matamshi makali dhidi ya wizi wa mali ya umma na aliamini kuwa hakuna taifa linaweza kustawi ikiwa viongozi hawawajibiki.
Nje ya Kenya, Raila alikuwa na ushawishi mkubwa barani Afrika. Kama Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika kuhusu Miundombinu, alitembea mataifa mengi kutafuta ushirikiano wa kimaendeleo na kuhimiza uunganishaji wa Afrika kupitia miundombinu ya kisasa.
Katika majukwaa ya kimataifa, sauti yake ilikuwa ya kipekee, ya kiongozi aliyeelewa changamoto za bara lakini pia mwenye maono ya kulivusha katika enzi mpya.
Kwa sababu hiyo, aliheshimiwa kama ‘Simba wa Afrika’, mtu ambaye alibeba maono ya bara zima kwenye mabega yake.
Raila ameacha urithi mkubwa ambao utadumu vizazi vingi:Alipigania uchaguzi huru na wa haki, alitetea haki za jamii zilizopuuzwa, aliongoza juhudi za maridhiano ya kitaifa kupitia handisheki zake na waliokuwa wapinzani wake na aliwaonyesha vijana kuwa siasa si lazima iwe ya ubinafsi bali ya huduma kwa umma.
Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf, alimtaja Raila kama “mwanasiasa mashuhuri wa bara la Afrika” na “Mwana wa Afrika aliyejawa na maono.”
“Raila Odinga alikuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya, na alikuwa mtetezi thabiti wa demokrasia, utawala bora na maendeleo yanayozingatia maslahi ya wananchi,” alisema Youssouf. “Dhamira yake ya miongo mingi ya kupigania haki, mfumo wa vyama vingi, na mageuzi ya kidemokrasia imeacha alama isiyofutika – si tu Kenya, bali kote barani Afrika. Ujasiri wake, uvumilivu, na imani yake katika mazungumzo na taasisi za kidemokrasia uliwavutia viongozi wengi, mimi nikiwa mmoja wao.”
“Akiwa Mwakilishi Maalum wa Muungano wa Afrika, Raila alifanya kazi kwa bidii kuendeleza ajenda ya kuunganisha na kuimarisha ushirikiano barani, juhudi zilizowezesha misingi ya Soko Huru la Bara la Afrika (AfCFTA) na mageuzi ya kijamii na kiuchumi kwa ujumla.”
“Afrika imepoteza mmoja wa wana wake waliokuwa na maono ya kina kiongozi aliyejitolea maisha yake kwa haki, demokrasia na mshikamano,” alisema Youssouf, akiongeza kuwa urithi wake utaishi kwa vizazi vingi vijavyo.
Katika maisha yake, Raila alichukiwa na wengi, lakini aliheshimiwa hata na maadui wake wa kisiasa. Leo, baada ya kuondoka duniani, dunia inakubali kuwa hakika alisimama upande wa haki.
Pengo aliloacha Raila Odinga haliwezi kupimwa kwa maneno au takwimu. Ni pengo la maono, ujasiri, na sauti isiyoogopa kusema ukweli.
Kenya na Afrika zimempoteza mpiganiaji wa haki, shujaa wa demokrasia, na kinara wa matumaini,” asema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki
Kaka yake Dkt Oburu Odinga, aliyeteuliwa kaimu kiongozi wa chama cha ODM, alikiri hawezi kujaza pengo aliloacha kaka yake mdogo.
“Nataka kushukuru chama changu, ODM, kwa kuniteua kuwa kiongozi wa chama. Ingawa viatu vya Raila ni vikubwa mno kuvitoshea, ninachotaka ni kujitahidi kadri ya uwezo wangu. Nitajitahidi,” Oburu alisema Ijumaa, wakati wa ibada ya kitaifa ya wafu ya Raila katika uwanja wa Nyayo.