Mayatima wa Raila kisiasa 2027 ikinukia
WABUNGE walipopiga foleni katika majengo ya bunge Ijumaa kutazama mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, baadhi yao walihisi kifo chake kama piga kuu katika mustakabali wao kisiasa.
Wengi wa wanasiasa hao, haswa kutoka eneo la Nyanza waliingia bungeni “kwa kushikwa mkono” kisiasa na mwanasiasa huyo mkongwe.
Ikumbukwe kwamba kwa zaidi ya miongo mitatu, Bw Odinga amekuwa mlezi wao kisiasa, alipoendeleza siasa za upinzani nchini.
Siasa hizo zilikuwa za aina yake kwani zilikita katika utetezi wa wanyonge, demokrasia ya vyama vingi, haki za kibinadamu na utawala bora.
Hii ndiyo maana alivutia imani ya raia wengi, hali iliyompa nguvu na hivyo kufuatwa hata na wanasiasa wa kizazi chake kama vile James Orengo na Peter Anyang’ Nyong’o, ambao wakati mmoja walidiriki kumpinga na wakajikwaa kisiasa.Wawili hao sasa ni magavana; Profesa Nyong’o akiongoza Kisumu, akihudumu muhula wa pili naye Bw Orengo alikihudumu kama gavana wa pili wa Siaya tangu kuanzishwa kwa utawala wa ugatuzi.
Wadadisi wanasema Orengo atakumbwa na kibarua kikubwa kutetea wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Hii ni kwa sababu marehemu Odinga alichangia pakubwa katika ushindi wake katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Katika eneo la Luo Nyanza, magavana kama vile Orengo wa Siaya, Ochilo Ayacko wa Migori na hata Gladys Wanga wa Homa Bay watatolewa kijasho 2027 watakapokuwa wakipambana kutetea viti vyao bila kivuli cha Raila,” anasema Martin Andati.
“Kuna uwezekano mkubwa kuwa hali kama hiyo itawakumba magavana wengine wa ODM wanaohudumu muhula wa kwanza kama vile Fernandes Barasa (Kakamega), Paul Otuoma (Busia), Abdulswamad Sheriff Nassir (Mombasa) na Gideon Mungaro (Kilifi) miongoni mwa wengine,” anaongeza.
Kauli yake inalandamana na ya mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora ambaye pia anatilia shaka uwezo wa kaimu kiongozi wa ODM Oburu Oginga kudumisha mshikamano katika chama hicho.
“Kwa mtazamo wangu, Oburu hana sifa za kisiasa ambazo Raila alikuwa nazo. Hana ushawishji miongoni mwa raia wa kawaida. Hii ndiyo maana itakuwa vigumu kwake kuheshimiwa na viongozi pamoja na wanachama wa ODM, sababu inayofanya wanasiasa waliomtegemea Raila kusalia mayatima wa kisiasa,” anaeleza mchanganuzi huyo ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Katika majengo ya bunge siku ya Ijumaa, kuna tapo la wabunge ambao walionekana kuachwa mayatima kufuatia kifo Raila.
Wao ni wale ambao wamekuwa watetezi wake wakubwa, kutokana na ukuruba wake na Rais William Ruto.
Kwenye orodha hii ni, wabunge; Peter Kaluma (Homa Bay Mjini), Millie Odhiambo (Suba Kaskazini), Otiende Amollo (Rarieda), Adipo Okuome (Karachuonyo) miongoni mwa wengine.Mbali na wabunge, tapo jingine la wandani wa Odinga waliobaki mayatima ni “wataalamu” wa ODM wanaohudumu kama mawaziri katika Serikali Jumuishi.Hawa ni Opiyo Wandayi (Kawi), Hassan Joho (Madini), John Mbadi (Fedha), Wycliffe Oparanya (Ustawi wa Vyama vya Kisiasa) na Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki Beatrice Askul.
Watano hawa walikuwa wakishikilia nyadhifa kuu katika ODM kabla ya Rais Ruto kuwatunukia nyadhifa hizo, Julai mwaka jana