Habari za Kitaifa

Nilinyimwa hata sekunde 90 kusema ukweli kuhusu Raila, asema Karua

Na BENSON MATHEKA October 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha People’s Liberation Party (PLP), Bi Martha Karua, amefichua kile angekisema iwapo angepewa fursa ya kuhutubu wakati wa mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, huko Bondo.

Bi Karua alisema ujumbe wake ungekuwa mfupi lakini wenye uzito mkubwa.

Akizungumza katika kipindi cha kisiasa kilichorushwa na runinga yaya KTN Jumanne, Oktoba 21, 2025, Karua alisema sekunde 90 zingemtosha kueleza maoni yake kuhusu demokrasia, utawala wa kikatiba, na maadili ambayo Raila aliyatetea maisha yake yote.

“Ningesema kuwa tulipigania demokrasia ya vyama vingi ambayo sasa imejumuishwa kwenye katiba, na kwa hivyo nitasalia katika upinzani. Upinzani utasalia kwa sababu katiba inaruhusu. Hivyo basi juhudi za kuleta vyama vyote chini ya paa moja ni kinyume na katiba,” Karua alisema.

Alisisitiza kuwa njia bora ya kumheshimu hayati Raila Odinga si kwa hotuba ndefu au ahadi za kisiasa, bali kwa kuendeleza vita vyake vya haki na demokrasia.

“Ningesema pia kuwa heshima kuu tunayoweza kumpa Raila ni kufuata maadili yake na kutetea mfumo wa vyama vingi, pamoja na haki za wananchi. Serikali lazima iachane na ukiukaji wa haki za watu, utekaji nyara, mateso na ukandamizaji wa aina yoyote,” aliongeza.

Karua, aliyekuwa mgombea mwenza wa Raila katika uchaguzi wa urais wa 2022 na mshirika wake wa muda mrefu katika kupigania demokrasia, alisema kuwa Raila alijitolea sana kwa uhuru wa kisiasa wa Kenya na anastahili kuheshimiwa kwa vitendo, si maneno tu.

Alisisitiza kuwa msimamo wake kuhusu siasa za upinzani unasalia kuwa dhabiti, akisema kuwa roho ya Raila ya kupigania demokrasia lazima iendelee hata baada ya kifo chake.

“Sikuhitaji zaidi ya sekunde 90 kuzungumza. Ukweli niliotaka kusema hauhitaji hotuba ndefu,” Karua aliongeza.

Kauli yake inajiri siku chache baada ya mazishi ya Raila huko Bondo, ambapo viongozi kutoka pande mbalimbali za kisiasa walikusanyika kumuenzi.

Alikosoa jinsi viongozi wa upinzani walivyotendewa wakati wa ibada za mazishi ya marehemu Raila, katika Uwanja wa Nyayo na baadaye Bondo.

Kwa mujibu wa Karua, ingawa serikali ilifanya vyema kumpa Raila mazishi ya kitaifa, haikuwa sawa kujaribu kumiliki hafla hiyo na kuwatenga viongozi wa upinzani.

Alisema Kenya ni taifa la vyama vingi, na kwa hivyo hafla yoyote ya kitaifa inapaswa kuonyesha ushirikishaji, kwani serikali inawakilisha raia wote, si wale wa serikalini pekee.

Alisema hali ilikuwa nafuu kidogo Bondo, ambako kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, alitaja majina ya baadhi ya viongozi wa upinzani, lakini bado hawakutambuliwa rasmi  na maafisa wa serikali.