• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 12:47 PM
Serikali yatakiwa ikinge wakulima dhidi ya soko huru la EAC

Serikali yatakiwa ikinge wakulima dhidi ya soko huru la EAC

Na MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Simon Mbugua ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Vyama vya Ushirika izindue mikakati ya dharura ya kuwakinga Wakenya dhidi ya athari hasi za biashara huru katika Jumuiya.

“Uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) matokeo yake ni soko huru. Hata hivyo, kuna shida moja ambapo Sarafu ya Kenya ni thabiti ikilinganishwa na sarafu katika mataifa wanachama. Ina maana kuwa, wafanyabiashara kutoka mataifa kama Uganda na Tanzania wanaleta mayai katika soko la Kenya na kuyauza kwa Sh8 kwa kila moja lakini shillingi hizo zikipelekwa Tanzania au Uganda na kubadilishwa, zinageuka kuwa faida za juu kwa wafanyabiashara hao,” akasema Bw Mbugua.

Alisema kuwa nao wafugaji kuku wa Kenya wakiwa sokoni wanalemewa kuuza mayai yao kwa Sh8 kwa kuwa gharama za uzalishaji ziko juu na wanauza wakitumia Shillingi ya Kenya ambayoi ndiyo wanatumia rasmi.

Bw Mbugua aliteta kuwa gharama ya kuzalisha yai moja hapa nchini iko katika kiwango cha Sh8 hivyo basi ile bei ya chini ambayo mfugaji wa kuku wa Kenya anaweza akauza yai moja ikiwa ni Sh10.

“Hiyo ndiyo sababu ninaomba serikali ya Kenya imakinike kwa kuwa soko la Kenya sasa limegeuka kuwa la kumhangaisha mkulima asili wa Kenya. Kusema kuna soko huru sio kumaanisha hakufai kuwa na mikakati ya kulainisha soko,” akasema.

Alisema kuwa kwa sasa wafanyabiashara wa Kenya wanazidi kuwekewa vikwazo katika mataifa ya Tanzania na Uganda, mataifa hayo yakijaribu kujikinga kutokana na ushindani usio na usawa huku Kenya ikiwa imefungua milango yake wazi bila masharati yoyote.

“Kuna masharti katika taifa la Tanzania kuwa kila bidhaa ambayo inaingizwa huko kutoka Kenya iwe imeelezea kwa kina kwa Lugha ya Kiswahili. Pendekezo hilo ni la kuwatatiza tu wafanyabiashara wa Kenya kwa kuwa utapata Kiswahili cha Tanzania sio cha Kenya na unaishia kuzimwa nafasi ya kuuza Tanzania,” akasema.

You can share this post!

KAULI YA WALIBORA: Msimamo wa Prof Ngugi kuhusu tija ya...

SEKTA YA ELIMU: Yakini, ufichuzi kwamba baadhi ya kozi...

adminleo