Raila Jr apakwa mafuta kuongoza familia ya babake
RAILA Odinga Junior ametawazwa rasmi kuchukua uongozi wa familia ya babake baada ya sherehe ya kitamaduni iliyofanyika nyumbani kwao eneo la Bondo, Alhamisi, Oktoba 23, 2025.
Hafla hiyo, iliyoongozwa na mjomba wake Dkt Oburu Oginga, ilibeba umuhimu mkubwa wa kitamaduni kwa familia hiyo, ikimaanisha kumkabidhi rasmi majukumu na mamlaka ya kifamilia kufuatia mazishi ya babake, aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Raila Amolo Odinga.
Dkt Oburu, ambaye ndiye kaka mkubwa wa Raila, alisema kuwa tukio hilo lilijikita sana katika mila za jamii ya Waluo, ambazo huelekeza jinsi familia hubadilisha uongozi baada ya kifo cha kiongozi wa boma.
Alisisitiza kuwa hafla hiyo haikuwa ya kisiasa, bali ni ya kimila, ya kukabidhi rasmi jukumu la uongozi wa nyumbani pamoja na baraka za kifamilia.
“Kiti cha mamlaka katika nyumba hii sasa kipo mikononi mwa Junior, pamoja na mama yake. Mama atakuwa hapo kumpa ushauri anaohitaji, lakini lazima asimame imara. Asimame imara na aongoze boma kwa mujibu wa utamaduni wetu,” alisema Dkt Oburu.
Alieleza kuwa ingawa Junior sasa ndiye kiongozi wa nyumba hiyo, familia kubwa ya Odinga bado ipo chini ya mamlaka yake ya kimila kama mzee mkuu wa ukoo.
“Huu si uongozi wa kisiasa, bali ni uongozi wa kifamilia. Familia pana ya Odinga ambayo mimi ndiye mwenyekiti wake, bado ipo chini yangu kama ilivyokuwa wakati wa baba yake kuhusu masuala ya kitamaduni,” aliongeza.
Kwa mujibu wa desturi za jamii ya Waluo, siku ya nne baada ya mazishi (chieng’ mar ang’wen) ndiyo siku rasmi ya kumaliza maombolezo.
Familia ilikusanyika kuadhimisha siku hiyo, ambayo kwa kawaida huashiria kufungwa rasmi kwa shughuli za mazishi na mwanzo wa awamu mpya kwa familia iliyopoteza mpendwa.
“Ndugu yangu alizikwa Jumapili iliyopita,” alieleza Dkt Oburu. “Ukihesabu kuanzia Jumapili hadi jana usiku, ni usiku wa nne. Katika tamaduni zetu, siku ya nne ndiyo siku maombolezo hufungwa rasmi.
Siku hiyo pia mabinti walioolewa hurudi makwao, na wana waliokuwa wakikaa hapa wakati wa maombolezo huruhusiwa kurudi kwa familia zao.”
Alisema familia hiyo ilifuata utamaduni ule ule uliotumika wakati wa mazishi ya baba yao, marehemu Jaramogi Oginga Odinga.
“Hatuwezi kupuuza mila,” alisema Dkt Oburu. “Hata katika Biblia kulikuwa na Isaka, Yakobo na Esau, baba aliwabariki wanawe. Vivyo hivyo katika tamaduni zetu, baraka na sherehe za kukabidhi mamlaka ni sehemu ya imani na utamaduni wetu.”
Sehemu kuu ya sherehe hiyo ilikuwa ibada ya kitamaduni ya kunyoa nywele, maarufu kama liedo.
Kitendo hicho huchukuliwa kama ishara ya utakaso, upya wa maisha, na mabadiliko kutoka kipindi cha maombolezo kwenda katika maisha mapya.
“Junior sasa atachukua uongozi wa familia pamoja na vyombo vyote vya mamlaka kama ishara ya nafasi yake mpya,” aliongeza Dkt Oburu.
Wazee walieleza kuwa hapo zamani, sherehe ya liedo ilikuwa mchakato wa kina unaofanywa kwa hatua.
Awali, wembe ulipitishwa vichwani mwa wajane na watoto, kisha baadaye kwa waombolezaji wengine.
“Zamani, ungeweza kusikia sauti ya wembe alfajiri,” alisema John Akumu, mzee kutoka Alego. “Ilikuwa sauti iliyotambulisha kuwa maombolezo yameanza rasmi kijijini. Siku hizi watu hufanya mara moja tu, au hata kwa alama ndogo tu nyuma ya kichwa.”
Sherehe hiyo pia ilihitimisha rasmi kipindi cha kuagana kwa waombolezaji.