Dereva wa Raila afunguka
MNAMO Januari 30, 2018, Kenya ilishuhudia moja ya matukio ya kisiasa yasiyosahaulika.
Katika bustani ya Uhuru Park, maelfu ya wafuasi walikusanyika kushuhudia Raila Odinga akiapa kama “Rais wa Wananchi.”
Asubuhi hiyo, Erick Ominde, dereva wa Raila, alipokea maagizo kwamba angempeleka kiongozi huyo wa upinzani kwenye bustani hiyo.
“Ilikuwa safari ngumu. Hakuna aliyejua nini kingetokea. Kulikuwa na vitisho vya kukamatwa. Ilihisi kama tunasafiri kuelekea historia, au hatari,” anakumbuka.
Walisafiri kupitia barabara ya Ngong hadi Kenyatta Avenue kuelekea Uhuru Park, ambako maelfu walikuwa wamekaidi onyo la polisi. Kutoka ndani ya gari, Ominde alitazama Raila akiinua Biblia na kuapa.
“Niliingiwa na hofu, lakini Raila aliniambia, ‘Kuwa jasiri, Erick. Kila kitu kitakuwa sawa.’ Maneno hayo yalinipa utulivu,” asema.
Baada ya kuapa, Raila aliwapungia mkono wafuasi wake kwa muda mfupi kisha akaondoka chini ya ulinzi mkali. Ominde aliongoza msafara huo kupitia njia za siri akiepuka maafisa wa polisi.
“Raila alijua kila njia ya mkato jijini Nairobi. Tulipitia Kenyatta Avenue, Valley Road kisha Upper Hill kuelekea Karen,” anaeleza.
Miaka mitano baadaye, Machi 2023, Ominde alijikuta tena akiendesha gari katikati ya moshi wa vitoa machozi na kelele za ving’ora wakati wa maandamano dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.
“Siku hiyo Raila alinimwagia maji kichwani na kuniambia, ‘Kuwa jasiri.’ Nilikanyaga mafuta gari nikapita katikati ya moshi na vurugu. Ni siku ambayo sitasahau,” anasema.
Kwa miaka 24, Ominde amekuwa nyuma ya usukani wa mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa zaidi nchini Kenya — akiona historia ikiandikwa mbele ya macho yake.
“Nimekuwa naye tangu akiwa Waziri wa Barabara, hadi akiwa Waziri Mkuu. Nimeona yote — ushindi, machozi na gesi ya machozi,” anasema.
Ominde mwenye umri wa miaka 43 kutoka Miwani, Kisumu, alikutana na Raila kupitia rafiki yake, Dkt Odongo Odiyo, aliyempendekeza kwa kazi hiyo.
“Nilipokutana na Baba kwa mara ya kwanza, alinichunguza kisha akasema, ‘Wewe utakuwa dereva wangu.’ Hapo ndipo maisha yangu yalibadilika,” anakumbuka.
Alianza kazi Raila akiwa Waziri wa Barabara, Ujenzi na Makazi (2003–2005). Hata hivyo, Raila alikuwa na historia ndefu ya upinzani, akiwa tayari amewahi kufungwa kwa miaka tisa katika utawala wa chama kimoja wa Moi.
“Alinifundisha njia zote za Nairobi. Aliniambia, ‘Njia ikifungwa, daima kuna nyingine.’ Maneno hayo yaliniongoza hadi leo,” asema Ominde.
Mwaka 2007, Raila aligombea urais lakini akashindwa na Mwai Kibaki, hali iliyosababisha machafuko ya baada ya uchaguzi. Wakati alipoingia serikalini kama Waziri Mkuu mwaka 2008, baadhi ya maafisa walitaka amwondoe dereva wake kwa sababu za itifaki, lakini Raila alikataa.
“Aliwaambia, ‘Huyu ndiye dereva wangu. Siwezi kumuacha.’ Hivyo ndivyo alivyokuwa mwaminifu kwa wanaomhudumia.”
Ominde anakumbuka jinsi Raila alivyojali maisha ya wafanyakazi wake.
“Kila asubuhi alikuwa akiuliza kama nimekula au familia yangu iko salama. Alimsaidia hata mke wangu kupata kazi,” asema kwa tabasamu.
Kazi yake haikuwa ya saa chache — ilikuwa maisha.
“Wakati wa kampeni, usingizi ulikuwa nadra. Tulitembea kaunti hadi kaunti bila kupumzika. Nilijifunza nidhamu na uvumilivu kutoka kwake,” asema.
Anakumbuka pia safari ya barabarani hadi Rwanda kupitia Uganda.
“Baba alikataa kutumia ndege. Alitaka kuona hali ya nchi. Tulipokuwa tukisafiri, aliniambia historia ya harakati za ukombozi barani Afrika. Ilikuwa kama kusafiri na kitabu cha historia hai,” anakumbuka.
Baada ya Raila kuingia kwenye ushirikiano wa kisiasa na Rais Ruto mwaka 2024, baadhi ya majukumu ya Ominde yalibadilika.
“Nilianza mara kwa mara kupeleka magari hadi Ikulu. Nidhamu niliyopata kutoka kwa Baba ilinisaidia kujibadilisha,” asema.
Leo, Erick Ominde ni mmoja wa madereva wa Ikulu ya Nairobi, lakini kumbukumbu za safari zake na Raila — kupitia moshi wa vitoa machozi, vurugu na historia — zinabaki moyoni mwake.
“Baba alinifundisha jambo moja muhimu: katika maisha, ukikwama, tafuta njia nyingine. Daima kuna njia nyingine,” asema.