Mtahiniwa kufanya KCSE rumande Lamu
MWANAFUNZI wa shule ya upili iliyo eneo la Lamu ya Kati, Kaunti ya Lamu, huenda akalazimika kufanya mitihani yake ya KCSE akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Hii ni kutokana na kuwa, alikamatwa na kuwekwa rumande kwa sababu ambazo hazijabainika. Wanafunzi wa Kidato cha Nne walianza KCSE Jumanne iliyopita, kwa mitihani ya Utendaji.
Wakati huo huo, mwanafunzi wa mtihani wa kitaifa wa Gredi ya Sita (KPSEA) kutoka Shule ya Faza Boys Comprehensive, Lamu Mashariki, alilazimika kufanya mtihani wake katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya King Fahd ambako amelazwa akipokea matibabu baada ya mkono wake kuvunjika.
“Ninafahamu kuwa kuna mwanafunzi amelazwa katika Hospitali ya King Fahd na amefanyiwa upasuaji kwenye mkono uliovunjika. Tumeandaa mipango ili aweze kufanya mtihani wake huko. Pia kuna mwanafunzi mwingine aliye rumande lakini tumefanya mipango ya haraka na naye anafanya mtihani akiwa huko. Hadi sasa kila kitu kinaendelea vizuri,” alisema Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti ya Lamu, Bw Zachary Mutuiri.
Mitihani ya KPSEA na KJSEA kitaifa ilianza jana (Jumatatu). Watahiniwa 36 wa KPSEA na KJSEA kutoka msitu wa Boni, Kaunti ya Lamu, walihamishiwa maeneo mengine kufanya mitihani hiyo.
Kulingana na Bw Mutuiri, hatua hiyo ilichukuliwa sababu kuu ikiwa ni shule husika kukosa idadi kamili ya angalau watahiniwa 15 wa KPSEA au KJSEA wanaohitajika kuwezesha taasisi zao kuorodheshwa kuwa vituo vya kujisimamia kufanya mitihani hiyo.
Kaunti hiyo ina watahiniwa 3,498 wa KPSEA ilhali wale wa KJSEA ni 4,432.
Katika Kaunti ya Tana River, Naibu Kamishna, Bw Andrew Mutua, alisema ingawa baadhi ya wanafunzi waliripotiwa kutoweka katika baadhi ya maeneo, hakuna mwanafunzi aliyesajiliwa atakayefanya mtihani hospitalini au gerezani.
“Hatutawaacha. Leo tunawatuma machifu kuhakikisha tunapata asilimia 100 ya wanafunzi wote kufanya mitihani,” alisema.
Kwa mujibu wa maafisa wa elimu, zaidi ya wanafunzi 5,000 wanafanya mitihani katika maeneo mbalimbali ya Kaunti ya Tana River.
Bw Mutua aliwahakikishia wazazi na wadau kuwa mitihani inaendelea kwa utulivu na serikali imejizatiti kuhakikisha mazingira ya haki na amani katika vituo vyote vya mitihani.
Huko Mombasa, manyunyu madogo hayakuathiri morali ya walimu na watahiniwa.
Mkurugenzi wa Elimu wa Kanda, Bi Anne Kiilu, aliwahimiza walimu kuendelea kuwahamasisha wanafunzi wote wakati wa kipindi hiki cha mitihani, akisema kuwa eneo hilo lina lengo la kuinua viwango vyake vya kitaaluma.
Kaunti ya Mombasa ina vituo 573 vya KPSEA vyenye jumla ya watahiniwa 27,498, na vituo 273 vya KJSEA vyenye watahiniwa 21,677.
Katika Kaunti ya Taita Taveta, Mkurugenzi wa Elimu wa Kaunti hiyo, Bw Khalif Hirey, alisema maandalizi yote yamekamilika kuhakikisha mitihani inafanyika kwa uwazi kote kaunti nzima.
Kaunti hiyo ina vituo 205 vya KPSEA na 194 vya KJSEA ambapo jumla ya watahiniwa 7,546 na 6,867 mtawalia wanakalia mitihani hiyo.
Ripoti za Kalume Kazungu, Stephen Oduor, Mishi Gongo na Lucy Mkanyika