Makundi ya haki yataka Bunge kuingilia kesi ya utekaji Wakenya wawili nchini Uganda
AMNESTY International Kenya, Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) na Vocal Africa wametangaza mipango ya kuwasilisha ombi kwa Bunge la Taifa na Seneti wakitaka hatua zichukuliwe kuhusu kutoweka kwa Wakenya wawili, Bob Njagi na Nicholas Oyoo, ambao hawajulikani walipo kwa zaidi ya siku 25 baada ya madai ya kutekwa nchini Uganda.
Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa jijini Nairobi hapo jana, mashirika hayo yalielezea hofu kuhusu kile walichokitaja “kutoweshwa kwa kulazimishwa.” Walisema wanaume hao wawili wanaripotiwa kushikiliwa katika mazingira duni bila matibabu, usaidizi wa kisheria au mawasiliano na familia zao.
“Tunazidi kushtushwa na ukimya na kutochukua hatua kwa Serikali ya Kenya. Wakenya hawa wanastahili kulindwa na katiba na kupata majibu ya haraka kuhusu hatima yao,” alisema Bw. Irungu Houghton, Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International Kenya.
Mkurugenzi Mkuu wa Vocal Africa, Bw. Hussein Khalid alisema utekaji huo unaonyesha tishio kubwa zaidi uhuru wa kiraia Afrika Mashariki kuzimwa. “Mateso yao si kuhusu wanaharakati wawili pekee, bali ni ishara ya kufungika kwa nafasi ya ushiriki wa wananchi. Hakuna serikali inayopaswa kuruhusu raia wake kutoweka bila maelezo,” akasema.
Mashirika hayo yalitaka uthibitisho kuwa wako hai, yakidai taarifa za kijasusi zinaonyesha wanateswa na afya yao inaendelea kuzorota. Yalibainisha kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya ilijishughulisha awali, lakini sasa imenyamaza, jambo linalozua maswali kuhusu dhamira ya serikali za Kenya na Uganda kulinda utawala wa sheria na raia wao.
Bw. Abner Mango kutoka LSK alimtaka Rais wa Uganda Yoweri Museveni kufichua walipo Njagi na Oyoo. “Serikali ya Uganda inapaswa kuhakikisha usalama wao, kuruhusu upatikanaji wa msaada wa kisheria, mawasiliano na familia zao na kuhakikisha ustawi wao. Pia, tunasisitiza uchunguzi wa wazi na kuwawajibisha waliohusika,” alisema.
Bw. Felix Wambua, ambaye ni Mratibu wa Kitaifa wa Free Kenya Movement, alisema wanaume hao walikuwa wakijihusisha sana na shughuli za utetezi. “Hili linaweza kumtokea yeyote kati yetu. Serikali zinapowanyamazisha raia mipakani, demokrasia yenyewe huwa hatarini,” alionya.
Zaidi ya Wakenya 300 tayari wameripotiwa kutumia baruapepe kwa Rais Museveni wakitaka hatua zichukuliwe. Amnesty International Kenya ilisisitiza kuwa mamlaka za Uganda lazima zijibu wito huu ili ahadi za haki za binadamu za kikanda ziwe na maana.
Njagi na Oyoo walisafiri Uganda mnamo Oktoba 1, 2025 kumuunga mkono mgombea wa urais wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine. Mashahidi walisema walitekwa karibu na kituo cha mafuta cha Kireka, karibu na Kampala, na wanaume wenye silaha waliovaa sare na nguo za kiraia, na kisha kulazimishwa kuingia kwenye gari. Hawajaonekana tangu wakati huo.
Mawakili waliwasilisha ombi la watu waliokamatwa kufikishwa katika Mahakama Kuu ya Kampala, lakini vyombo vya usalama vya Uganda vilikana kuwakamata. Jeshi la Uganda (UPDF) na Polisi ya Uganda walisema hakuna rekodi zinazoonyesha wanawashikilia. Jaji aliwatangaza kuwa “watu waliopotea” na akashauri ripoti rasmi ziwasilishwe.
Makundi ya haki za binadamu yalipinga madai hayo, yakinukuu mashahidi na uwezekano wa kushikiliwa kwa siri katika vituo vya kijeshi ambako visa vya mateso vimeripotiwa awali. Amnesty International Kenya ililinganisha kisa hicho na matukio ya zamani ya kutekwa nyara katika eneo hilo.
Tukio hilo limeongeza hofu kuhusu kuongezeka kwa uhasama dhidi ya watetezi wa haki za binadamu Afrika Mashariki. Kwa familia za wanaume hao, kila siku bila majibu inaongeza uchungu. “Tunatarajia serikali yetu kusimama kidete kwa ajili ya watu wake. Maisha ya Wakenya ni muhimu Kampala kama yalivyo Nairobi,” alisema Bw. Houghton.