Oburu sasa ndiye bosi wa ODM, aidhinishwa na Kamati Kuu ya Usimamizi
ASASI kuu ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) imemwidhinisha Seneta wa Siaya Oburu Oginga kuwa kiongozi mpya wa kitaifa.
Mkutano wa Kamati Kuu ya Usimamizi (CMC) wa chama hicho uliofanyika Jumatatu, Oktoba 27, 2025, uliamua kuwa Dkt Oburu alijaze nafasi hiyo iliyosalia wazi kufuatia kifo cha kakake, Raila Odinga, Oktoba 15, 2025.
Seneta huyo wa Siaya, ambaye ni kakake mkubwa wa Raila, aliteuliwa kuwa kaimu kiongozi wa ODM mnamo Oktoba 16, siku moja baada ya Raila kutangazwa kuaga dunia akipokea matibabu nchini India.
Uamuzi ulifikiwa katika mkutano wa dharura wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) ya ODM uliofanyika, Nairobi.
“Katika mkutano huu wa kwanza wa kamati hii tangu kifo cha kiongozi wa chama, asasi kuu imemtawaza Mheshimiwa Dkt Oburu Oginga kuwa kiongozi mpya wa chama cha ODM. Kamati ya CMC inatoa wito kwa maafisa na wanachama wa ODM kumuunga mkono na kushirikiana naye kumwezesha kuongoza chama wakati huu mgumu,” Katibu Mkuu Edwin Sifuna akasema kwenye kikao na wanahabari baada ya mkutano huo uliodumu kwa saa nne katika jumba la Dusit, jijini Nairobi.
ODM sasa inalenga kutumia uidhinishwaji wa Oburu kushinikiza wanachama wake kudumisha umoja baada ya hofu kwamba kinaweza kugawanyika kutokana na kutokuwepo kwa Raila.
Wakati wa mkutano wa Oktoba 27, 2025, chama kiliwahakikishia wafuasi wake kwamba hali ni shwari huku kikishutumu vyombo vya habari kwa kueneza habari za kutopotosha kwamba ODM inaelekea kupasuka “vipande”.