Babu Owino na Makamu wa Rais wa LSK wataka mawaziri wazimwe kuchapa siasa
MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino na makamu wa rais wa Chama cha Mawakili Nchini (LSK) Mwaura Kabata wamefika kortini wakitaka Mawaziri wazimwe kushiriki kampeni za kisiasa.
Wawili hao wanasema kwa kushiriki siasa mawaziri wanakiuka hitaji kuu la afisi yao linalowahitaji kutopendelea kwa misingi ya kisiasa na kuonekana kuwahudumia Wakenya wote kwa usawa.
Aidha, Mbw Babu na Kabata wanataka mahakama kuu ibaini kuwa sehemu ya 25 ya Sheria ya Mgongano wa Kimamlaka ya 2025 ni kinyume cha Katiba.
Kulingana na kesi hiyo, sehemu hiyo ya sheria inawaruhusu mawaziri wa serikali ya kitaifa na wale wa serikali za kaunti kupinga au kuunga mkono masilahi ya chama Fulani cha kisiasa au kushirikisha katika shughuli za kisiasa zinazoweza kuonekana kuathiri hitaji la afisi za kuonekana kutopendelea.
“Kwamba sehemu hiyo ya sheria inakinzana na Kipengele cha 75 cha Katiba ya Kenya, kinachohitaji kwamba Maafisa Wakuu wa Serikali wanafaa kuonyesha mienendo ambayo haionyesha mgongano wa masilahi yao ya kibinafsi nay ale ya umma au majukumu yao rasmi,” kesi hiyo inasema.
Mbw Babu na Kabata wanasema kutozuiwa kwa mawaziri wa serikali na wale wa serikali za kaunti kushiriki siasa kunabagua maafisa wengine wa serikali ambao wanazuiwa kushiriki katika shughuli za kisiasa.
Walalamishi hao wawili wanadai kuwa zaidi ya mawaziri 20 wa serikali ya kitaifa wamenaswa na vyombo vya habari wakishiriki kampeni za kisiasa huku wakisaka uungwaji mkono kwa wagombeaji wa vyama mbalimbali vya kisiasa katika chaguzi ndogo zilizoratibiwa kufanyika Novemba 27, 2025.
“Kwamba kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, Mahakama hii inaombwa kutoa agizo la kuzuia kutumika kwa Sehemu ya 25 ya Sheria ya Mgongano wa Kimasilahi Nambari 11 ya 2025,” Bw Kabata alisema katika kesi hiyo.
Walalamishi hao walisema mamlaka ambayo mawaziri na maafisa wakuu wa serikali wamepewa ni kwa manufaa ya umma na inapasa kuendeleza uaminifu wa afisi hizo machoni pa umma. Wanaongeza kuwa maafisa wote wakuu wanao wajibu wa kuwatumikia wananchi, bali sio kuendeleza mamlaka ya kuwatawala.
Mbw Babu na Kabata wanataja kisa cha Aprili 2, 2025 wakati wa mkutano wa kisiasa ulioongozwa na Rais William Ruto Kieni, Nyeri ambapo ilidaiwa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alitoa kauli iliyoashiria kuhusisha Shirika la Huduma kwa Polisi (NPS) na siasa.
Kesi hiyo inaeleza kuwa sehemu ya 23 (2) ya Sheria ya Utawala Bora na Maadili ya 2012 inawazuia Maafisa wa Serikali kushiriki shughuli za kisiasa ambazo zinaweza kuingilia hitaji lao na kutoonyesha mapendeleo kisiasa kwa heshima ya afisi wanazoshikilia.