Maoni

MAONI: Wakuu wa ODM wasiruhusu Ruto kulemaza chama chao

Na CHARLES WASONGA October 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SASA sio siri tena kwamba, Rais Willam Ruto anatamani zaidi kutwaa udhibiti wa chama cha ODM kufuatia kifo cha Raila Odinga ili kufanikisha ajenda yake ya kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.

Kisiasa, ni sawa kabisa kwa Dkt Ruto kuwa na ndoto kama hiyo kwa sababu kila rais anayedumu muhula wa kwanza hutamani kupata fursa ya kuendelea muhula wa pili.

Hii ni katika muktadha wa Kenya yenye Katiba inayomzuia rais kuhudumu kwa zaidi ya mihula miwili ya miaka mitano kila moja.

Kwa upande mwingine, mrengo wa upinzani mkuu pia ungetaka kupata uungwaji mkono kutoka kwa ODM, au sehemu ya wafuasi wake, ili ufanikishe ajenda yake ya kumwondoa Ruto mamlakani 2027.

Hii ndio maana wakati wa ibada ya mazishi ya marehemu Odinga iliyofanyika Bondo, Siaya, Oktoba 19, Dkt Ruto aliweka wazi kwamba hataruhusu ODM kurejeshwa katika siasa za kucheza karata za upinzani.

Alieleza kwamba, “kwa heshima ya Raila nataka kuwahikikishia kuwa ODM itaunda serikali ijayo au itakuwa mshirika katika serikali ijayo.”

Uongozi wa sasa wa ODM unafaa kuchanganua kauli hii kwa undani zaidi kuzuia uwezekano wa Rais Ruto kutwaa ‘usimamizi’ wa chama hicho kufanikisha ajenda zake za kisiasa.

Usemi wa Ruto ulisheheni hatari kulemaza ODM, kwa kuchochea migawanyiko na migongano kati ya viongozi wake, alivyokifanyia chama cha Jubilee baada ya Uhuru Kenyatta kumpokeza mamlaka ya kuongoza nchi Septemba 13, 2022.

Aidha, anaweza kupanga njama ya kufanikisha kumezwa kwa ODM na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) sawa na chama cha Amani National Congress (ANC) kilichoongozwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Isitoshe, viongozi wa ODM, kama vile Gladys Wanga, ambao wameleweshwa nauchu wa kutaka kuendelea kusalia serikalini, wanapaswa kufahamu kuwa ni Rais Ruto ambaye Januari 2023 alipendekeza kuwa vyama vyote tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza vivunjwe na wanachama wote wajiunge na UDA.

Hii ni kinyume na kipengele cha 4 (2) cha Katiba kinachosema kuwa Kenya taifa lenye demokrasia ya vyama vingi na kipengele cha 38 kinachompa kila Mkenya haki ya kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa anachokitaka bila kushurutishwa na yeyote.

Ni kwa sababu hii ambapo, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, ambaye ni kiongozi wa Ford Kenya, alikatalia mbali pendekezo la Rais Ruto.

Alishikilia kwamba chama cha Ford Kenya kitasalia kuwa chama huru huku kikishirikiana na vyama vingine katika muungano wa Kenya Kwanza.