Habari

Joho apambana asizimwe kushikilia wadhifa wa umma

Na PHILIP MUYANGA October 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Madini, Uchumi wa Baharini na Masuala ya Bahari, Hassan Joho, ameomba Mahakama Kuu mjini Mombasa itupilie mbali ombi lililowasilishwa dhidi yake likitaka atangazwe kuwa hafai kushikilia wadhifa wowote wa umma nchini.

Kupitia wakili wake, Bw Joho alisema kuwa ombi hilo lililowasilishwa mwaka 2021 na mfanyabiashara Ashok Doshi na mkewe Pratibha, linategemea uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi (ELC) ambao ulibatilishwa na Mahakama ya Rufaa.

“Ombi hili halina msingi wowote wa kisheria. Msingi wake umejengwa juu ya mchanga unaoteleza, kwa hivyo lazima litupwe,” wakili wa Bw Joho aliambia mahakama Jumanne.

Bw Doshi na mkewe walimshtaki Bw Joho pamoja na Mwakilishi wa Wadi ya Changamwe, Bernard Ogutu, kwa kutotii amri ya mahakama iliyozuia Serikali ya Kaunti ya Mombasa isiingie katika kipande cha ardhi kinachomilikiwa na wanandoa hao.

Mnamo mwaka 2021, Mahakama ya Ardhi iliwapata Bw Joho na Bw Ogutu na hatia ya kudharau mahakama na kuwatoza faini ya Sh250,000 na Sh20,000 mtawalia.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa, kupitia uamuzi wake wa Novemba 2024, ilifuta hukumu hiyo, ikibaini kuwa Bw Joho hakukabidhiwa binafsi notisi ya kesi hiyo, na kwamba walalamishi walishindwa kuthibitisha madai yao kwa viwango vinavyotakikana kisheria.

Licha ya hilo, wakili wa wanandoa hao aliambia mahakama kuwa ombi lao halikutegemea tu uamuzi wa Mahakama ya Ardhi, akimshutumu Bw Joho kwa kujaribu “kufupisha mchakato wa kisheria”.

“Ombi letu halijajengwa tu juu ya uamuzi wa ELC. Je, ni nini kinachomfanya mshtakiwa wa kwanza kuwa na hofu kiasi cha kutaka kuzuia kesi isisikizwe?” akauliza wakili huyo.

Wanandoa hao walisema kuwa Bw Joho na Bw Ogutu, wakiwa maafisa wa umma, walipaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji, lakini kwa kudharau amri ya mahakama, walikiuka maadili ya uongozi na utawala bora yaliyowekwa na Katiba.

Bw Joho, ambaye hapo awali alikuwa Gavana wa Mombasa, alisema kuwa amekuwa akitoa maelezo kuhusu suala hilo kila mara anapoteuliwa kushika wadhifa wa umma.

Mahakama Kuu imesema itatoa uamuzi wake Machi 6, 2026, kuhusu iwapo itaondoa kesi hiyo au la.