Jinsi mvulana wa Grade ya 3 aliokoa maisha katika ajali ya Murang’a
MVULANA mwenye umri wa miaka tisa katika kaunti ya Murang’a ametajwa kama shujaa kwa kuwaokoa abiria tisa katika ajali iliyotokea katika Mto Kiama Jumamosi usiku na iliyosababisha vifo vya watu sita, watano wakiwa kutoka familia moja.
Watu hao walikuwa wakisafiri kutoka Kiambu kwa shughuli ya ulipaji mahari matatu waliokuwa wakisafiria ilipotumbukia kwenye mto huo.
Kando na watu sita waliokufa, wengine tisa walijeruhiwa.
Boniface Njoroge, ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Msingi ya Gatunguru, alikuwa ameandamana na wazazi aliweza kuruka kutoka kwa gari hilo lilipokuwa likizama majini na kukimbia hadi kituo cha kibiashara cha karibu kutafuta usaidizi.
Kwa kufanya hivyo alisaidia kuwaokoa abiria wengine waliokuwa ndani ya matatu hiyo akiwemo mamake, Bi Alice Wangechi.
Hata hivyo, babake Boniface, Paul Karanja ni miongoni mwa abiria sita waliokufa.
Katika kijiji cha Ndia, kilichogubikwa kwenye majonzi, tulimpata Boniface akicheza na wenzake.
Na tulipomuuliza kilichofanyika, mvulana huyo ambaye alionekana kutofahamu thamani ya kitendo chake akasema:
“Tulikuwa tukisafiri kurejea nyumbani ndipo matatu ikatumbukia ndani ya mto huo. Na maji yalipokuwa yakiingia ndani, niliweza kuruka nje na kukimbia hadi katika kituo cha kibiashara cha Chomo kuitisha usaidizi. Nilikutana na mwendesha boda boda na nikamjulisha kilichotokea na ndipo akapiga kamsa. Watu walikimbia hadi katika mto na kuwaokoa wale ambao walikuwa wamekwama ndani ya gari.”
Bw Wangechi alisema alipopata ufahamu, alikuwa akielea kwenye maji na fikra iliyomjia ni kwamba mwanawe wa kiume alikufa. Lakini baadaye aligundua kwamba ni mtoto huyo, Boniface, aliyewaokoa.

Akielezea matukio baada ya ajali hiyo, Bi Wangechi alisema walinusurika kutokana na neema za Mungu. Hii ni licha ya kwamba alimpoteza mumewe Paul Karanja.
“Bonie alikuwa ameketi nyuma pamoja na mvulana mwingine na sikujua kwamba alifaulu kuruka nje. Muda mfupi baada ya kuokolewa nilianza kupiga mayowe, nikiuliza aliko mtoto wangu. Niliambiwa kuwa ni yeye alikuwa ameenda kutafuta watu wa kutusaidia,” mama huyo akaeleza.
Wengine waliokufa ni pamoja na wanandoa, Peter Mwangi na mkewe Alice Wambui, Elijah Kamau na Amos Kiharu na mwanamke mmoja ambaye hakutambuliwa na aliyepewa lifti na dereva.
Abiria mwingine aliyenusurika, Bw Peter Gachuru aliyeketi karibu na dereva, alimsifu mvulana kwa hatua yake ya haraka iliyowaokoa.
“Eneo ambako ajali ilitokea huwa halina makazi na hivyo mtoto Boniface alikimbia kwa umbali wa kilomita mbili hadi kituo cha kibiashara cha Chomo. Kama haingekuwa mvulana huyo jasiri aliyeruka nje na kuwapasha watu kuhusu kisa hicho, tungekufa maji,” akasema.