Pigo tena kwa Waititu korti ikikataa kumpunguzia dhamana
MAHAKAMA Kuu imekataa ombi la aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Kiambu, Ferdinand Waititu kwamba apunguziwe dhamana ya Sh53.5 milioni, hatua iliyomzuia kupata uhuru wake huku akiendelea kukata rufaa dhidi ya adhabu ya ufisadi.
Mahakama iliamua kwamba Waititu alishindwa kutoa sababu za kutosha za kubadilisha masharti ya mahakama iliyomtaka kutoa dhamana kamili ya benki, masharti ambayo yeye mwenyewe ndiye aliyependekeza.
Gavana huyo wa zamani anaendelea kufungwa katika gereza la Kamiti, akitumikia kifungo cha miaka 12 baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh53.5 milioni aliyoamriwa kulipa kufuatia hukumu ya kushiriki ufisadi.
Waititu na washtakiwa wenzake wanne walipatikana na hatia mnamo Februari 2025 kuhusiana na kashfa ya ujenzi wa barabara ya thamani ya Sh588 milioni iliyotokea wakati wa utawala wake.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilithibitisha madai ya utoaji zabuni kwa njia isiyo halali na mgongano wa maslahi.Hii ni mara ya pili mwaka huu kwa Waititu kushindwa kupata dhamana.
Mnamo Machi 2025, Mahakama Kuu ilikataa ombi lake la awali, ikitaja hatari yake kutoroka na uzito wa makosa yaliyofanya apatikane na hatia.
Hata hivyo, mwezi Julai 2025, mahakama ilikubali ombi lake baada ya kuahidi kutoa dhamana ya benki ya kiasi kamili cha faini.
Katika kikao cha Oktoba, wakili wake aliomba mahakama imhurumie, akisema kwamba mteja wake ana matatizo ya kifedha na alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.
Aliomba dhamana hiyo ibadilishwe kuwa hati za kumiliki mashamba au dhamana ya kawaida, au kupunguzwa hadi Sh20 milioni, kwa sababu haingewezekana kupata dhamana ya benki.Hata hivyo, mahakama ilisema mlalamishi (Waititu) mwenyewe ndiye aliyesema kuwa angepata dhamana ya benki.
“Alifahamu masharti na gharama zake, na alikubali kuzifuata. Sasa hawezi kubadilika na kudai kuwa hawezi kutimiza masharti hayo.”
Upande wa mashtaka ulidai kuwa Waititu anatumia ujanja kuchelewesha rufaa yake, ambayo ilipangwa kusikilizwa Machi 2025 lakini haijakamilika hadi sasa.
Mahakama ilikumbusha kuwa, kwa mujibu wa agizo lililotolewa Septemba 17, 2025, rufaa hiyo lazima ikamilishwe ndani ya siku 120 kuanzia Oktoba 1, 2025, ikionya kwamba ucheleweshaji zaidi unaweza kusababisha rufaa kufutiliwa mbali.Kwa uamuzi huu, uhuru wa Waititu sasa unategemea kutoa dhamana ya benki ya Sh53.5 milioni.
Akishindwa kufanya hivyo, ataendelea kubaki gerezani hadi rufaa yake itakaposikilizwa na kuamuliwa kikamilifu.