Habari MsetoSiasa

Mzozo wa urithi wa mali katika familia ya Nyong'o watokota

February 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RUSHDIE OUDIA

MZOZO wa urithi wa mali katika familia ya Prof Anyang’ Nyong’o umechukua mkondo mpya baada ya kesi hiyo kupelekwa katika Mahakama ya Rufaa, kupinga uamuzi uliowajumuisha wapwa wake kuwa miongoni mwa watakaonufaika.

Prof Nyong’o na dadake, Dkt Risper Nyagoy wanataka uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kuwajumuisha wapwa wao kama warithi kuondolewa. Wawili hao tatari wameshtakiwa kwa kukaidi agizo la mahakama kufika mbele yake. Nyong’o ndiye gavana wa Kaunti ya Kisumu.

Mahakama ilikuwa imemjumuisha mmoja wa wapwa wao kama msimamizi-mwenza wa mali hiyo ya mamilioni ya pesa inayomilikiwa na babu yao. Wawili hao pia walikuwa wameagizwa kutoa vitabu vya taarifa za fedha kuhusu mali hiyo.

Kwenye uamuzi aliotoa mnamo Oktoba 11, 2018, Jaji Thripsisa Cherere alifutilia mbali barua na stakabadhi zilizomtaja Prof Nyong’o na Dkt Nyagoy kama wasimamizi wakuu wa mali hiyo.

Mahakama ilimjumuisha Bw Kenneth Okuthe kama msimamizi-mwenza. Mali hiyo inakadiriwa kuwa yenye thamani ya Sh200 milioni.

Mali inayozozaniwa inajumuisha shamba la ekari 100 lililo katika eneo la Miwani na nyumba kadhaa zilizo katika Barabara ya Jogoo, Nairobi.

Ardhi nyingine zimo katika maeneo ya Manyatta, Tamu, Milimani na Raba Mashariki katika Kaunti Ndogo ya Seme, Kaunti ya Kisumu.

Wawili hao wanaitaka Mahakama ya Rufaa kusimamisha utekelezaji wa uamuzi huo hadi pale rufaa yao itakaposikizwa.

Wawili hao walieleza kutotosheka kabisa na uamuzi huo. Walisema kwamba wanaamini kwamba rufaa yao itafaulu, hivyo lazima wangoje hadi itakaposikizwa na kuamuliwa.

Kulingana na wakili wa Prof Nyong’o, Jefferson Museve, watawasilisha rufaa mpya, baada ya kuondoa ya awali waliokuwa wamewasilisha katika Mahakama Kuu.

“Tunaona kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa rufaa tuliyowasilisha katika Mahakama Kuu kufaulu. Hivyo, tunaitaka kusikizwa hadi kukamilika,” akasema Bw Museve.

Bw Okuthe alikuwa akiitaka mahakama kuwahukumu Prof Nyong’o na dadake miezi sita kila mmoja kwa kukiuka kanuni zake.