Habari

Upinzani waapa kuonyesha serikali kivumbi chaguzi ndogo

Na KEVIN CHERUIYOT November 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

VIONGOZI wa Umoja wa Upinzani Novemba 3, 2025 walitangaza kuwa watatumia njia zote kushinda chaguzi ndogo ambazo zimeratibiwa kufanyika Novemba 27.

Viongozi hao walisema kuwa watahakikisha kwamba UDA na ODM ambazo zipo ndani ya Serikali Jumuishi zinalemewa kwenye chaguzi hizo.

Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alisema kuwa vyama tanzu ndani ya upinzani vimekubali kuungana na kuwasilisha mwaniaji mmoja katika chaguzi hizo za ubunge na udiwani.

Bw Gachagua alisema kuwa mfumo ambao waliutumia kufikia mwaniaji wa ubunge ndio ule ule ambao watautumia kuafikia mwaniaji wa kumwangusha Rais William Ruto mnamo 2027.

“Kitakachofanyika kwenye chaguzi hizi ni maandalizi ya kura ya 2027. Nawahakikishia Wakenya ije mvua au jua, tutakuwa na mwaniaji moja imara wa kumwaangusha Rais Ruto 2027,” akasema Bw Gachagua.

Bw Gachagua pia alikashifu tamko la rais kuwa atawafagia wapinzani wake wote mapema katika uchaguzi mkuu wa 2027 akiaashiria utakuwa mswaki kwake.

“Sisi si wapinzani wake, wapinzani wake ni Wakenya na sisi tunafanya tu kile Wakenya wanataka tufanye. Tuna amri kutoka kwa Wakenya tuibuke na mwaniaji bora wa kumwangusha Rais Ruto,” akaongeza.

Awali vyama hivyo vilikubaliana kuwaunga mkono Newton Karish wa DP (Mbeere Kaskazini), Seth Panyako wa DAP-Kenya (Malava) kisha jana Wiper ilimwondoa mwaniaji wake na kuahidi kumuunga mkono Stanley Kenga wa DCP (Magarini).

Bw Kenga sasa atapambana na aliyekuwa mbunge wa Magarini ambaye ushindi wake ulifutwa Harrison Kombe.

Pia Wiper ilikubali kumuunga mkono mwaniaji wa DCP katika wadi ya Narok Mjini.