Maoni

Mpango wa “One Health Initiative” ni bora katika kuzuia magonjwa

Na CHARLES WASONGA November 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MNAMO mwaka wa 2001 viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Africa (AU) walikongamana jijini Abuja, Nigeria, kujadili njia ya kukabiliana na changamoto zinazokumba sekta ya afya katika bara hili.

Viongozi hao walikubaliana kwamba ili Afrika iweze kufikia malengo yake ya kimaendeleo, serikali za nchi zinapaswa kupambana na magonjwa yanayoathiri binadamu.

Katika kile kilichojulikana kama Azimio la Abuja la 2001 (Abuja Declaration of 2001) walikubaliana kwamba kiasi cha asilimia 15 ya bajeti za nchini, kila mwaka, zitengewe sekta ya afya kufadhili mipango ya kuzuia na kutibu aina mbalimbali za magonjwa sugu yanayosibu wanadamu.

Magonjwa yaliyotambuliwa kero wakati huo yalikuwa kama vile; Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Lakini baada ya miaka mataifa wanachama wa AU, ikiwemo Kenya, yalishindwa kutimiza malengo ya azimio hilo, kutokana na sababu kadhaa kama vile usimamizi mbaya wa fedha za umma.

Nchi hizo zimekuwa zikitenga bajeti finyu zaidi kwa sekta za afya, hali inayozifanya kutegemea ufadhili kutoka nchi na mashirika fadhili.

Utegemeaji huo wa usaidizi kutoka nje sasa umechangia Kenya na nchi zingine za Afrika kutumbukia katika changamoto kubwa tangu mapema mwaka huu.

Hii ni baada ya Rais wa Amerika Donald Trump kuzima ufadhili ambao shirika la Amerika la kufadhili maendeleo kimataifa (USAid) limekuwa likifadhili mipango ya kupambana na magonjwa kama Ukimwi, malaria na kifua kikuu.

Athari za hatua hiyo ya Trump imeanza kujitokeza nchini Kenya kwani ripoti zinasema kuwa wagonjwa wa Ukimwi wanateseka kwa kutopata dawa za kupunguza makali (ARVs) na huduma nyinginezo muhimu.

Ni kwa msingi huu ambapo ipo haja ya kuzuia maambukizi ya magonjwa mbalimbali yanayoathiri binadamu na yanayosababishwa na mtagusano na wanyama katika mazingira mbalimbali.

Kwa hivyo, nakubaliana na Chama cha Matatibu Nchini (KMA) na Chama cha Madaktari wa Mifugo (KVA) kwamba mzigo wa gharama ya matibabu utapungua ikiwa juhudi za kuzuia magonjwa katika binadamu na wanyama zitaendeshwa kwa pamoja.

Vyama hivi vimeanzisha mpango mzuri unaojulikana kama “One Health Initiative” unaotoa mafunzo na uhamasisho kuhusu umuhimu wa kuzuia magonjwa yanayotokana na mtagusano kati ya watu, wanyama na mazingira yao.

Mpango kama huu ni muhimu kwa sababu, utafiti umeonyesha kuwa asili ya magonjwa kama Ukimwi na Covid-19 ni wanyama.

Virusi vya Ukimwi vilitoka kwa nyani kabla ya kusambaa kwa binadamu huku virusi vya corona vikisemekana kuishi kwa mara ya kwanza ndani ya Popo walioishi China.

Isitoshe, magonjwa mengine hatari kama malaria na yale ya kuambukiza, yanayo uhusiano mkubwa na mazingira ambamo wanadamu wanaishi.

Kero la mabadiliko ya tabia nchi, linaloshuhudia nchini Kenya na mataifa mengine ya ulimwengu, pia limebainika kuchochea mlipuko wa magonjwa mbalimbali yanayoathiri wanadamu.

Kwa hivyo, vyama vya KMA na KVA vishirikishe wadau wote vinapoendesha uhamisho chini ya mwavuli wa mpango wa “One Health Initiative” katika mwezi huu wa Novemba.

Kwa mfano, vishirikishe serikali za kaunti, mashirika ya kijamii (CBOs), mashirikia ya kidini (FBOs) na makundi mengine katika kongamano la mwaka huu ili kufanikisha ajenda muhimu ya kuzua magonjwa.