Habari

Fumbo mwili wa mwalimu aliyeuawa TZ ukikosa kupatikana

Na KASSIM ADINASI November 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA ya mwalimu Mkenya aliyeuawa wakati wa vurugu za uchaguzi Tanzania imeshindwa kupata mwili wake.

Celestine Ogutu, dada mkubwa wa John Okoth Ogutu, aliyefariki mikononi mwa maafisa wa usalama wa Tanzania na ambaye alikuwa wa mwisho kuzungumza naye anasema hawajaweza kupata uliko mwili wa mpendwa wao.

Okoth alikuwa akifundisha katika shule ya Sky School jijini Dar es Salaam.

Celestine alisema mnamo Oktoba 29, alipotazama habari kuhusu ghasia zilizozuka wakati wa uchaguzi nchini humo, mawazo yake yalielekezwa moja kwa moja kwa kakake mdogo aliyekuwa na umri wa miaka 33, aliyekuwa akifundisha katika shule hiyo kwa zaidi ya miaka minane.

“Nilimpigia mamangu kwanza kuuliza kama alikuwa amesikia jambo lolote kutoka kwa ndugu yangu Okoth. Mama akanijibu, ‘Sijasikia kutoka kwake, tafadhali tafuta mwanangu’ na tukamaliza mazungumzo,” alisema Bi Ogutu nyumbani kwao Kademba A, Pap Gori, Alego Usonga.

Aliendelea: “Mara moja nilijaribu kuwasiliana na ndugu yangu kupitia WhatsApp, kwa kawaida tunawasiliana kupitia mitandao ya kijamii. Nilimtumia ujumbe mfupi, ‘Bro, uko salama?’ lakini hakujibu. Nilijaribu tena kwa nambari yake nyingine, kwa kuwa alikuwa na nambari mbili; moja ya Kenya na nyingine ya Tanzania.”

Kutokana na kuzimwa kwa intaneti Tanzania, aliona alama tu kwenye ujumbe wake jioni hiyo.

Siku iliyofuata, Oktoba 30, akiwa karibu kuingia kanisani kwa ibada ya usiku, alipokea simu kutoka nambari isiyojulikana iliyoanza na +255, ambayo ilikuwa imejaribu kumpigia mara kumi.

“Kabla sijaingia kanisani, niliamua kurudisha simu. Sauti upande wa pili ilikuwa dhaifu na yenye uchovu — ilikuwa ya binamu yangu mkubwa. Aliniuliza kama nilikuwa najua kilichotokea. Nilidhani labda mama yangu ndiye alikuwa amefariki, lakini alinipasha kuwa ndugu yangu ndiye aliyekuwa ameuawa na maafisa wa usalama wa Tanzania,” alisema Bi Ogutu.

Baadaye alipata maelezo kutoka kwa rafiki wa ndugu yake aliyeshuhudia tukio hilo lote.

“Aliniambia kuwa jioni ya Oktoba 29, ndugu yangu alienda kituo cha biashara cha Gaba, Dar es Salaam, karibu na alikokuwa akiishi. Maafisa wa usalama waliokuwa wakituliza maandamano waliwakamata na kuwafyatulia risasi, na wengi waliuawa papo hapo,” alisema.

Rafiki huyo aliweza kumpigia binamu yao simu mara moja miili bado ikiwa eneo la tukio.

“Kulingana naye, kulikuwa na miili kadhaa na maafisa waliendeleza doria kwa zaidi ya saa mbili wakilinda maiti hizo. Baada ya hapo, miili yote ilipelekwa mochari ya Mwananyamala,” akaongeza.

Baada ya kupata taarifa za kifo cha ndugu yake, Bi Ogutu alianza kupanga uwezekano wa kuhamisha mwili wake Kenya kwa mazishi.

Kupitia rafiki huyo na uongozi wa Sky School, familia ilijaribu kupata mwili wa ndugu yao.

Kwa mshangao wao, waligundua kuwa mwili wa ndugu yao na wengine waliodaiwa kuuawa haikuwepo katika mochari ya Mwananyamala.

“Inaumiza sana kujua kwamba hata baada ya kuuawa, mwili wake haujulikani ulipo. Niliwaagiza waliokuwa wakitafuta waangalie kwa makini, nikawapa maelezo ya sura yake. Lakini walisema mochari ilikuwa ikihifadhi miili miwili tu — ya mzee mmoja na mtoto — waliorekodiwa kufariki wakati wa maandamano,” alisema kwa huzuni.

Bi Ogutu anaomba Wizara ya Masuala ya Kigeni kuingilia kati ili kusaidia kubaini ukweli kuhusu mahali mwili wa mpendwa wao upo.

“Maumivu ya kumpoteza kijana katika nchi ya kigeni, na sasa kutopata mwili wake, ni makubwa mno. Mama yangu mzee anaumia sana. Mwaka jana tulimpoteza ndugu mwingine aliyekuwa akisoma chuo kikuu, mwezi Mei tulimzika baba yetu, na sasa kaka yetu mdogo ameondoka,” alisema kwa uchungu.

“Rafiki wa ndugu yangu alinieleza kuwa huenda miili hiyo ilitupwa kwenye kaburi la pamoja kuficha tukio au baharini au mtoni,” aliongeza Bi Ogutu huku machozi yakimtoka.