Habari

Wabunge waonya wananchi kuhama maeneo yanayokabiliwa na hatari ya maporomoko na mafuriko

Na CHARLES WASONGA November 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMATI ya Bunge la Kitaifa kuhusu Maendeleo ya Kikanda  Novemba 5, 2025 ilitoa wito kwa raia wanaoishi katika maeneo hatari kuhama ili kuzuia vifo vinavyotokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Aidha, kamati hiyo imetoa wito kwa serikali kutekeleza mikakati ya muda mrefu wa kuzuia majanga hayo huku ikiomba jamii ya kimataifa, sekta ya kibinafsi na wahisani kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa mikasa hiyo katika Elgeyo Marakwet ambako watu 34 walikufa.

Maeneo mengine yaliyoathiriwa na janga hilo lililosababishwa na mvua kubwa ni: eneo la Kimende (Kaunti ya Kiambu), Tinderet (Nandi), Kamutungi (Embu) na maeneo kadhaa ya Tana River na Kisumu.

“Tunawaomba raia wanaoishi katika maeneo hatari kutokea maporomoko na mafuriko kuwa waangalifu huku serikali kupitia Shirika la Kitaifa la Kusimamia Majanga (NDMU) ikiongoza shughuli za usambazaji wa misaada, kuwahamisha watu na kuwasaidia walioathirika. Wakome kuvuka barabara iliyojaa maji, mito na madaraja,”  mwenyekiti wa kamati hiyo Peter Lochakapong, akawaambia wanahabari katika majengo ya bunge.

Mwenyekiti huyo, ambaye ni mbunge wa Sigor, pia aliwataka raia kuondoka katika maeneo ya milima na maeneo tambarare ambayo hukumbwa na maporomoko ya ardhi na mafuriko kila mara.

“Kwa hivyo, kamati hii inawataka wananchi hao kushirikiana na maafisa wa mashirika ya kushughulikia majanga na wanawaomba kuondoka maeneo hatari. Wafuatilie ripoti zinazotolewa kila mara na Shirika la Utabiri wa Hali ya Anga, Wizara ya Usalama na Asasi za Serikali za Kaunti zilizotwikwa wajibu wa kushughulikia majanga,” akaongeza.

Bw Lochakapong alikuwa ameandamana na naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Liza Chelule (Mbunge Mwakilishi wa Nakuru), Basil Robert (Yatta), Paul Abuor (Rongo) na mbung wa Voi Khamis Abdi Chome.

Wabunge hao pia waliahidi kuweka presha kwa wabunge na maseneta ili wapitishe Mswada wa Kushughuli Majanga ambao unashughulikiwa na Kamati ya Upatanishi.