Habari

Oburu mbioni kusaka amani na kuwaunganisha wanachama

Na JUSTUS OCHIENG November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAIMU kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Dkt Oburu Oginga, ameanza juhudi za haraka za kurejesha umoja na utulivu ndani ya chama hicho,

Seneta huyo wa Siaya anajaribu kuwaleta pamoja wanachama waliokuwa waasi na vijana waliokuwa wakionyesha dalili za kukosa imani na uongozi wa sasa.

Katika hatua ambayo wachambuzi wa siasa wanaitaja kuwa “marekebisho ya kimkakati” kwa ODM baada ya kipindi cha misukosuko ya ndani, Dkt Oginga ameanzisha mikutano ya faragha na viongozi vijana na wakongwe, kwa lengo la kujenga umoja na uthabiti wakati ambapo chama kinapitia kipindi cha mabadiliko baada ya kifo cha mwanzilishi wake, Raila Odinga.

Kwa wiki kadhaa sasa, Seneta huyo amekuwa akifanya mazungumzo ya chini kwa chini na viongozi wa chama, wakiwemo wabunge na wanaharakati vijana wanaohusishwa na vuguvugu jipya la kisiasa linaloitwa Kenya Moja.

Vuguvugu hilo linaongozwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna, na linawajumuisha wabunge vijana kama Babu Owino (Embakasi Mashariki), Caleb Amisi (Saboti), na Anthony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini).

Pia, limepata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi wa vyama vingine, akiwemo mbunge wa Githunguri Gathoni wa Muchomba (UDA).

Kundi hilo limejitangaza kama “mrengo wa tatu” katika siasa za taifa, likijitenga na upande wa serikali unaoongozwa na Rais William Ruto na pia upinzani unaoongozwa na viongozi kama Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua.

Wanasema wanakusudia kubadilisha siasa za Kenya kuwa mashindano ya vizazi, wakiahidi mageuzi makubwa ifikapo uchaguzi wa 2027.

Katika mahojiano maalum na Taifa Leo, Dkt Oginga alithibitisha kuwa tayari amekutana rasmi na Bw Babu Owino kujadili njia za kuimarisha umoja ndani ya chama.

“Nimefanya kikao na Mheshimiwa Babu Owino. Tulijadili umuhimu wa kuimarisha umoja na ujumuishaji ndani ya ODM,” alisema. “Babu anaakisi ari, nguvu na matumaini ya vijana wetu. Ana mustakabali mzuri, na tuko imara pamoja,” alisema.

Dkt Oginga, ambaye ni kakaye marehemu Raila Odinga, sasa anajikuta katika juhudi za kusawazisha maslahi ya makundi mbalimbali ndani ya ODM, kuhakikisha chama hakitetereki baada ya kuondoka kwa kiongozi wake, huku pia akihakikisha vijana hawahisi kutengwa.

Amethibitisha kuwa mazungumzo yake hayahusishi tu Bw Owino, bali pia Bw Sifuna na Naibu Kiongozi Mwenza wa ODM, Godfrey Osotsi, ambao kwa miezi ya hivi karibuni wamekuwa wakitoa tahadhari kuhusu kuunga serikali ya Rais Ruto.

“Majadiliano haya si kuhusu vyeo au makundi,” alisema Dkt Oginga.

“Ni kuhusu umoja. Ni kuhusu kuwaleta wote kwenye meza moja. Hatuwezi kuruhusu tofauti ndogo zitugawanye wakati chama kinahitaji kuendelea pamoja.”

Seneta huyo alikiri kwamba kumekuwa na mvutano wa wazi ndani ya ODM katika miezi ya hivi karibuni, ukichochewa na mijadala kuhusu urithi wa uongozi wa Raila Odinga na mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi wa 2027.

“Mimi ninaamini vijana wanapaswa kuchukua nafasi zao za uongozi, ndio maana mimi huitwa kiongozi wa vijana.”Hata hivyo, Dkt Oginga alikanusha madai kwamba kuna mgawanyiko wa kizazi ndani ya ODM, akisisitiza kuwa “viongozi wa zamani” hawana nia ya kuwatenga vijana.