Habari

Jowi! Ni ng’ombe 100 Kalonzo akirudi kutoa heshima za mwisho kwa Raila Bondo

Na BENSON MATHEKA NA KASSIN ADINASI November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Wiper Democratic Movement, Kalonzo Musyoka Novemba 6, 2025 alifika kwa kishindo Opoda Farm, Bondo kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Hayati Raila Amollo Odinga.

Akiwa amevaa nguo za rangi ya kijani na kubeba mkuki na ngao, Kalonzo aliongoza msafara wake kumuenzi kiongozi huyo mashuhuri ambaye alikuwa mshirika wake wa kisiasa tangu uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2013.

Katika ishara ya mshikamano na heshima ya kitamaduni, msafara wa Wiper pia ulipeleka ng’ombe 150 kwa familia ya Odinga, ishara inayowakilisha mshikamano na heshima wakati wa majonzi.

Makamu rais huyu wa zamani aliandamana na Gavana wa Machakos Wavinya Ndeti, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jr., wazee wa Ukambani, wataalamu, viongozi wa dini, wabunge wa zamani na wa sasa, pamoja na wanachama wa Wiper Democratic Movement.

Msafara wao uliondoka Kisumu mapema asubuhi ya Alhamisi na kutua kwanza nyumbani kwa familia ya Raila huko Opoda kabla ya kuelekea Kango Ka Jaramogi, ambapo kiongozi huyo wa ODM amezikwa.

Kalonzo alisema alivaa mavazi ya rangi ya kijani kama ishara ya kisiasa kumuenzi Raila kama “baba wa maandamano”, akimpongeza kwa kupigania uhuru wa kidemokrasia Kenya kupitia maandamano ya amani. Alisema kuwa rangi ya kijani ilikuwa ni ishara ya ushujaa, upinzani, na moyo wa kupigania haki za wananchi.

“Leo nimekuja kuomboleza ndugu yangu, Raila Amollo Odinga, ambaye tulishirikiana naye kupigania nchi hii kuwa taifa lenye heshima na kidemokrasia,” alisema Kalonzo. Aliongeza kuwa, licha ya changamoto nyingi za kisiasa zilizokumba taifa, kila kizazi cha Wakenya kitasalia kuenzi jitihada za Raila za kupigania uhuru wa raia.

Akizungumza na vyombo vya habari Kisumu, Kalonzo alisisitiza kuwa Raila alipenda taifa, alitoa maisha yake kuhakikisha Kenya inakuwa taifa zuri, lenye heshima, na linalotilia mkazo demokrasia.

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa maisha ya kisiasa ya Raila yatabaki mfano wa kuigwa, hasa kwa vijana wanaojiandaa kuchukua nafasi za uongozi katika siasa za Kenya.

Msafara wake ulimtembelea Gavana Anyang’ Nyong’o wa Kisumu kabla ya kuelekea Bondo.

Kalonzo pia alimpongeza wakazi wa Kisumu na Siaya kwa ukarimu na mshikamano walioonyesha kwa Mama Ida Odinga na familia ya Odinga.

“Tumekusanyika kuomboleza ndugu yetu. Nimezungumza na Gavana James Orengo, na naona watu wa Kisumu na Siaya wamekutana nasi kwa moyo wote. Kila mmoja yupo hapa kuunga mkono Mama Ida na familia,” alisema.

Aidha, viongozi wa Wiper walisisitiza kuwa sherehe ya kuomboleza Raila ni nafasi ya kusherehekea urithi wake wa kidemokrasia, huku wakiahidi kuendeleza mapambano ya haki za raia na demokrasia iliyoanzishwa na kiongozi huyo.

Mnamo Jumatano, chama kilisema ziara hiyo ilikuwa ya Wiper pekee na kukanusha ripoti zilizokuwa zikisema kuwa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, angekuwa miongoni mwa watakaoambatana na Kalonzo.

Katibu Mkuu wa Wiper, Shakilla Abdallah, alisema kuwa ziara hii ina umuhimu mkubwa kisiasa kutokana na historia ya ushirikiano kati ya Wiper na Orange Democratic Movement (ODM).

Jana, Bw Musyoka alisema kwamba Bw Gachagua atafanya ziara yake Bondo kumuenzi Raila.

Musyoka na Raila walikuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka mingi, na uhusiano huo uliendelea hata baada ya kuwepo kwa serikali jumuishi iliyowaweka pande tofauti kisiasa.

“Raila na Kalonzo walikuwa wakiwasiliana kabla ya kifo cha Raila kwa sababu uaminifu wake umethibitishwa na wadau mbalimbali wa kisiasa. Ndio sababu anaonekana kuwa ndiye anayestahili kuungwa mkono na ODM na viongozi wengine,” alisema Abdallah.

Katibu Mkuu wa chama aliongeza kuwa licha ya Odinga kuchagua serikali jumuishi, “Musyoka alituomba tuendeleze heshima kwake kama Baba yetu.” Odinga daima alizungumza kwa heshima kuhusu Musyoka, ambaye alikuwa mgombea mwenza wake wa urais mara mbili mwaka 2013 na 2017, na alimsaidia pia wakati alichagua Martha Karua kama mgombea mwenza katika uchaguzi wake wa mwisho.